Ghasia hizo zimehusisha mashambulizi ya risasi kati ya wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Kipalestina – pamoja na matumizi ya tingatinga katika kambi za wakimbizi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20, jambo ambalo limeharibu huduma za umma, ikiwemo miundombinu muhimu ya umeme na maji.
Waziri wa vita wa Israel alisema Jumapili kuwa vikosi vinaweza kubaki katika kambi hizo kwa “mwaka ujao”.
Philippe Lazzarini, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), amesema “hofu, mashaka, na huzuni vimetanda tena. Kambi zilizoathirika zipo katika hali mbaya. Uharibifu wa miundombinu ya umma, kubomoa barabara, na vizuizi vya upatikanaji wa huduma ni mambo ya kawaida,” amesema.
Zaidi ya watu 50, wakiwemo watoto, wameuawa tangu uvamizi wa kijeshi wa Israel uanze wiki tano zilizopita, shirika la Umoja wa Mataifa limesema, likionya kuwa Ukingo wa Magharibi “unageuka kuwa uwanja wa vita” ambapo raia wa kawaida wa Kipalestina ndio wanaoteseka zaidi. Wakati huohuo, ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) pia imelaani “mbinu hatari na zenye sura ya kivita” zinazotumiwa na jeshi la Israel dhidi ya jamii za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.OCHA imethibitisha vifo zaidi vya raia na watu wengi kukosa makazi baada ya uvamizi wa kijeshi wa Israel wa siku mbili katika mji wa Qabatiya, kaskazini mwa wilaya ya Jenin, uliomalizika Jumatatu.
Wapalestina walikamatwa wakati wa operesheni hiyo, OCHA imebainisha, huku ikirejelea wasiwasi wake mkubwa kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya raia na ongezeko la mahitaji ya misaada kwa watu waliopoteza makazi.
Utawala katili wa Israel ulianza mashambulizi yake katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu baada ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas mnamo Januari 15. Operesheni hiyo katika Ukingo wa Magharibi ni moja ya kubwa zaidi tangu Intifada ya Pili ya Wapalestina katika miaka ya 1990.
342/