4 Machi 2025 - 23:28
Source: Parstoday
China yajibu mapigo dhidi ya ushuru mpya wa Trump

China imetangaza kujibu mapigo ya ushuru uliotangazwa dhidi ya nchi hiyo na Rais Donald Trump wa Marekani.

Siku ya Jumanne China ililipiza kisasi ushuru mpya wa Marekani, kwa kutangaza ongezeko la 10% -15% la ushuru kwa bidhaa mbalimbali za kilimo na chakula za Marekani.

Beijing pia imeyawekea vikwazo makampuni ishirini na tano ya Marekani kwa uuzaji wa nje na uwekezaji kwa misingi ya usalama wa taifa.

Makampuni kumi kati ya haya 25 ya Marekani yamelengwa na China kwa kuiuzia silaha Taiwan, ambayo China inadai kuwa ni eneo lake.

Ushuru huu wa kulipiza kisasi wa China umekuja wakati ambao ushuru wa 10% wa Rais wa Marekani Donald Trump umewekwa na umeanza kutekelezwa leo Machi 4 kwa bidhaa kutoka China. Hilo linafanya ushuru jumla kufikia 20%.

Trump anasema ni kwa sababu China haichukui hatua za kuzuia mtiririko wa dawa za kulevya kutoka China zinazoingia Marekani.

Wachambuzi wamesema Beijing bado ina matumaini ya kufikia makubaliano na utawala wa Trump, lakini ushuru wa kulipiza kisasi unatishia kuenea vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo makubwa ya kiuchumi.

Baada tu ya Trump kutangaza ushuru huo China ilitangaza Jumapili kuwa "inapinga vikali" ushuru uliowekwa na US dhidi ya Beijing, na kusisitiza kuwa itachukua "hatua zinazolingana ili kulinda kwa uthabiti haki na masilahi ya China."

Wataalamu wa masuala ya biashara, ujasiriamali na uwezekaji wanasema kuwa, uamuzi wa serikali ya Marekani wa kutoza ushuru wa juu kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Canada, Mexico, na China utawadhuru zaidi Wamarekani.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha