5 Machi 2025 - 22:45
Source: Parstoday
Mkutano wa London, maonyesho ya nguvu na uungaji mkono kwa Ukraine bila dhamana ya utekelezaji

Siku mbili baada ya kufedheheshwa Rais Zelensky wa Ukraine katika Ikulu ya White House na suala hilo kuakisiwa pakubwa kimataifa, viongozi wa nchi 19 za Ulaya, Canada na maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya na muungano wa NATO wamekutana mjini London kwa ajili ya kutangaza mshikamano wao na Ukraine katika vita vyake na Russia.

Keir Starmer, Waziri Mkuu wa Uingereza alizungumza mwishoni mwa mkutano huo kuhusu mpango wa hatua nne za ushirikiano na Ukraine kwa ajili ya kumaliza vita na kujilinda dhidi ya Russia. Kauli mbiu ya mkutano wa London ilikuwa "Kudhamini Mustakabali Wetu". Katika miaka themanini iliyopita, hakujawahi kuwa na tofauti kubwa kama inavyoshuhudiwa hivi sasa kati ya washirika wa pande mbili za Bahari ya Atlantiki kuhusu moja ya vitisho vikubwa vinavyoikabili Ulaya.

Serikali za Ulaya sasa zimetambua kwamba uhusiano na Washington uliodaiwa kujikita katika misingi ya kuaminiana na uungaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa demokrasia ya Magharibi katika kipindi cha miaka themanini iliyopita, sasa unakaribia kusambaratika. Viongozi wa Ulaya wanafikiria zaidi kuhusu umuhimu wa kuanzisha mfumo wa ulinzi wa pamoja, usiotegemea Marekani wala NATO. Linalojadiliwa sasa ni namna ya kuwa na muundo huru wa "nyuklia" wa kuzuia hujuma ya adui.

Hata Ujerumani, ambayo haina silaha za nyuklia, inazungumzia uwezekano wa kujitoa chini ya mwavuli wa nyuklia wa Marekani na kuwa chini ya ulinzi wa nyuklia wa Ufaransa na Uingereza. Iwapo mipango hiyo itatekelezwa bila shaka itabadilisha mfumo wa hivi sasa wa uwiano wa nguvu kimataifa baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Onyesho la kufedheheshwa Zelensky siku ya Ijumaa katika Ikulu ya White House kwa hakika lilikuwa dhihirisho la dharau kwa Umoja wa Ulaya. Mkutano wa viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya, Kanada, Umoja wa Ulaya na NATO huko London kwa hakika ulikuwa jibu kwa udhalilishaji huo dhidi ya Zelensky, ambapo wametangaza kuiunga mkono kikamilifu Ukraine. Zelensky aliwaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kwamba sasa anahisi nchi yake ina uungwaji mkono mkubwa.

Katika mkutano wa London, ilikubaliwa kuwa msaada wa kijeshi uendelee kutumwa Ukraine, Kiev iwepo katika mazungumzo yoyote ya amani na Russia, Ulaya ijaribu kuzuia uwezekano wa hatua za baadaye za Russia dhidi ya Ukraine na "muungano wa waliojitolea" uundwe kusaidia na kudhamini amani ya Ukraine baada ya kufikiwa makubaliano ya amani.

Ursula von der Leyen, Rais wa Tume ya Ulaya, pia alitangaza baada ya mkutano huo kwamba Umoja wa Ulaya unahitaji kujizatiti kwa silaha na kwamba nchi wanachama zinapasa kujiandaa kifedha ili kuongeza bajeti ya ulinzi. Alisisitiza kuwa Ulaya lazima pia iionyeshe Marekani kuwa iko tayari kutetea demokrasia. Pamoja na hayo, viongozi wa Ulaya wanajua kwamba bila ya uratibu na Marekani, hawawezi kujiondoa kwenye msuguano wa kisiasa ambao Trump ameuanzisha kuhusu jinsi ya kumaliza vita huko Ukraine. Ni kwa msingi huo ndio maana viongozi hao bado wanazungumzia kujenga daraja na kurejesha uhusiano na Marekani.

Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Italia, ambaye ana uhusiano wa karibu na mrengo wa Trump, alikuwa na mkutano wa pande mbili na Starmer kabla ya mkutano huo. Ameonya kuwa nchi za Magharibi ziko hatarini kugawanyika na kusisitiza nafasi ya Italia na Uingereza kuwa waunganishi wa Ulaya na Marekani inayoongozwa na Trump.

Viongozi wa Ulaya wanajikuta kwenye "njia panda kihistoria". Kwa upande mmoja, wanataka kumalizika vita hivyo haraka iwezekanavyo na kwa upande mwingine, hawataki amani ya kutwishwa ambapo yule anayedaiwa kuwa ni mchokozi atazawadiwa kutokana na misimamo yake. Katika mkutano wa London, viongozi wa Ulaya hawakutangaza ratiba yoyote ya kutekeleza ahadi walizotoa kuhusiana na Ukraine.

Tangu mwanzo, mgogoro wa Ukraine umekuwa na wahusika wawili muhimu ambao ni Russia na Marekani. Bila uwepo wa nchi mbili hizi, nafasi ya serikali za Ukraine na Ulaya, zikiwemo za Uingereza na Italia, ambazo zina uhusiano wa karibu na Trump, haina umuhimu wowote. Trump anafanya mazungumzo na Russia bila kujali maoni ya serikali ya Ukraine na za Umoja wa Ulaya. Wachambuzi wengi wanasisitiza kuwa, kutokuwepo mwakilishi wa Marekani katika mazungumzo ya London kunamaanisha kuwa hayana dhamana yoyote ya utekelezaji hasa kuhusiana na masuala ya usalama na kijeshi.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha