15 Machi 2025 - 21:55
Source: Parstoday
Mustakbali uliogubikwa na kiza wa Syria; wafuasi wa al Julani wazidi kuua raia

Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria limeripoti habari ya kuuawa zaidi ya raia 1,383 wasio na hatia katika shambulio lililofanywa na magenge yenye mfungamano na watawala wa hivi sasa wa Syria kwenye maeneo ya Waislamu wa Kishia, magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu.

Siku ya Jumatano, Shirika la Kufuatilia Haki za Binadamu la Syria lilitangaza idadi ya karibuni kabisa ya raia waliouawa kwenye mashambulio yaliyofanywa na maafisa usalama wa Hay'at Tahrir al-Sham kwenye eneo la pwani la Syria la magharibi mwa nchi hiyo. Shirika hilo lilisema watu 1,383 wasio na hatia wameuawa. Shirika la Kufuatilia Haki za Binadamu la Syria pia liliripoti habari ya kuweko uwezekano wa kuzikwa wahanga wa jinai hiyo kwenye makaburi ya umati, magharibi mwa Syria.

Wafuasi wa watawala wa hivi sasa wa Syria wameelekeza ukandamizaji wao dhidi ya raia wa kawaida katika hali ambayo wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wanatumia fursa hiyo kuzidi kuteka maeneo ya kusini mwa Syria.

Mustakbali uliogubikwa na kiza wa Syria; wafuasi wa al Julani wazidi kuua raia

Hii ni kusema kuwa, siku ya Jumatano, wanajeshi vamizi wa wa Israel waliingia katika maeneo mapya ya mkoa wa Quneitra kusini magharibi mwa Syria. Wanajeshi hao wa utawala unaokikalia kwa mabavu Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, waliingia katika mji wa Jabata al-Khashab nje kidogo ya mkoa wa Quneitra kusini-magharibi mwa Syria ikiwa ni kuendelea kutumia vibaya udhaifu wa watawala wapya wa Syria katika kulinda ardhi za nchi hiyo. Waziri wa Vita wa Israel, Israel Katz ametangaza kuwa, jeshi la utawala huo dhalimu limejiadaa kuweko nchini Syria kwa muda mrefu usiojulikana.

Uvamizi wa utawala wa Kizayuni nchini Syria unaendelea kiasi kwamba, vyombo vya habari vya Syria vimeripoti kuwa, jana Alkhamisi asubuhi pia, wanajeshi wa Israel waliingia kwenye maeneo mengine ya Syria wakiwa na zana za kivita na hakuna dalili za kuondoka nchini humo. Vyombo hivyo vya habari vimeongeza kuwa, baada ya wanajeshi vamizi wa Kizayuni kuingia katika miji ya Ain al-Nuriya na Kom Muhairis katika mkoa wa Quneitra nchini Syria, milio ya risasi nzito ilisikika kwenye maeneo hayo.

Matukio hayo yamepelekea kuzuka wimbi jipya la wakimbizi ambapo maelfu ya Waalawi wa Syria wanaendelea kukimbilia katika nchi jirani ya Lebanon.

Serikali ya Lebanon imethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa maelfu ya wakimbizi wa Syria wameshaingia Lebanon kupitia vivuko visivyo rasmi kufuatia mauaji dhidi yao yanayofanywa na maafisa usalama wa serikali ya al Julani.

Mustakbali uliogubikwa na kiza wa Syria; wafuasi wa al Julani wazidi kuua raia

Hali inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku kiasi kwamba, katika ripoti yake ya hivi karibuni, Umoja wa Mataifa umesema kuwa, maafisa wa serikali mpya ya Syria wameua familia nzima nzima bila ya kubakisha hata mtu mmoja wa familia hizo, ikiwa ni kuendeleza mauaji ya kizazi dhidi ya raia hao wa Syria. 

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza habari hiyo Jumatano na kuongeza kwamba baadhi ya familia nzima, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto wadogo; wote wameuliwa na vikosi vya serikali ya al Julani katika eneo la pwani la Syria. Thamin Al-Khaitan, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa amesema: "Kuna matukio mengi ya kutisha. Familia nzima, ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto na wale ambao hawakuweza kupigana, wameuawa, huku miji na vijiji vingi vya watu wa jamii ya Alawi vikilengwa kwa makusudi kwenye mashambulizi hayo." 

Hayo yanajiri huku duru mbalimbali za habari zikiripoti jana Alkhamisi kuwa mapigano yamezuka kati ya vikosi vya usalama vya serikali ya mpito ya Syria na vikosi vya Walinzi wa Pwani ya kusini-magharibi mwa nchi hiyo. Shirika la Habari la Al-Ma'luma la Iraq limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa mapigano makali yamezuka kati ya vikosi vya al Julani na Vikosi vya Walinzi wa Pwani huko Tartous, kusini magharibi mwa Syria.

Matukio haya yanazidi kutia nguvu matamshi ya wachambuzi wa mambo kwamba, mustakbali wa Syria umegubikwa na kiza totoro.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha