Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA -: Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa leo hii tarehe 15 / 03/ 2025 amezindua Msikiti wa Masjid Jaami’u Nuuril Hikma uliopo mtaa wa Yombo, Temeke jijini Dar _es_ Salaam, uliojengwa na Al-Hikma Foundation.
Mheshimiwa Kasim Majaliwa, akizungumza baada ya kuzindua Msikiti huo, alitoa wito kwa jamii ya Waislamu wa Watanzania watakaotumia na kufaidika na Msikiti huo kuhakikisha wanautunza na kuuhifadhi vizuri, kwa kuwa kufanya hivyo ni njia moja wapo ya kudumisha Ukaribu na Uhusiano Mzuri baina ya Mja na Mwenyezi Mungu (s.w.t), bali hilo linahesabika kuwa ni sadaka.
Aidha amesema kwamba: Msikiti ni Nyumba ya Mwenyezi Mungu, na ni Kituo cha kiroho, kijamii na kiutamaduni, na vile vile ni nyumba makhsusi kwa ajili ya Waislamu kufanya ibada mbalimbali ndani yake. Zaidi ya hilo Msikiti ni sehemu Tukufu kwa Waumini ambapo wanaweza kuutumia katika kuchuma elimu na maarifa, na hatimaye kujenga jamii bora inayojali na kujituma katika kutoa huduma za kijamii.
Katika Hafla hii ya Ufunguzi wa Msikiti huu, Shakhsia mbalimbali zimehudhuria, ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dokta Abubakar Zuber Ali Mbwana, ambaye amesema katika Hotuba yake kuwa: "Maendeleo sio ugomvi bali ni kufanya mambo yanayoonekana na yanayompendeza Mwenyezi Mungu ikiwemo ujenzi wa Msikiti ambao ni Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu".
Your Comment