Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani uamuzi huo uliochukuliwa na Marekani na Umoja wa Ulaya wa kupiga marufuku matangazo ya Televisheni ya al Aqsa na kusema, hatua hiyo ni jaribio la kuzima sauti za Wapalestina na kuwazuia kuwasiliana na ulimwengu wa nje. Imesema: Hatua hii inalenga kukandamiza uhuru wa kujieleza na kunyamazisha majukwaa yanayofichua sura halisi ya ugaidi uliopangwa na Wazayuni.
Taarifa ya Hamas imesisitiza kuwa: Hatua ya Marekani dhidi ya Televisheni ya al Aqsa ni uamuzi ulio kinyume na sheria dhidi ya vyombo huru vya habari vya Palestina vinavyofichua kwa jamii ya kimataifa mateso ya Wapalestina na jinai za Wazayuni.
Hamas pia imevitaka vyombo vya habari na mashirika ya habari ya kimataifa kulaani uamuzi huo na kutonyamaza kimya mbele ya hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu.
Televisheni ya Satalaini ya Al-Aqsa pia imetoa taarifa na kutangaza kuwa, kufuatia uamuzi wa pamoja wa Marekani na nchi za Ulaya, matangazo ya televisheni hiyo yamesitishwa katika satalaiti zote za kimataifa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni yoyote ya satalaiti itakayoendelea kurusha hewani matangazo ya Televisheni ya "Al-Aqsa" itakabiliwa na vikwazo vizito vya kifedha. Pia, mashtaka ya "kuunga mkono ugaidi" yatafunguliwa dhidi ya wasimamizi wa satalaiti zinazoiweka televisheni hiyo kwenye orodha zao za matangazo.
Al-Aqsa imelaani uamuzi huo, na kuutaja kuwa ni sehemu ya juhudi zilizoratibiwa za kukandamiza vyombo vya habari vya Palestina. Idara ya televisheni hiyo imesisitiza kuwa, hatua hizo zinachukuliwa sambamba na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Sauti ya Palestina.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, pia amezungumza katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa (Machi 14) kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu. Iravani amelaani mwenendo unaoongezeka wa kueneza chuki dhidi ya Waislamu na kusema: Chuki dhidi ya Uislamu ni chombo kinachotumiwa kuhalalisha uvamizi na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. Akizungumzia nafasi ya vyombo vikuu vya vya habari na mitandao ya kijamii katika kueneza chuki dhidi ya Uislamu, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: "Mitandao hiyo ya propaganda haiwalengi tu Waislamu, bali pia inachafua mapambano halali wa watu wa Palestina kwa kuchochea mazingira ya chuki."
Chuki dhidi ya Uislamu inazidi kuchukua sura mpya kila siku barani Ulaya na Marekani na imesababisha hujuma dhidi ya Uislamu, yaani mashambulizi ya kivitendo dhidi ya Uislamu na Waislamu. Wimbi kubwa na lililopangwa la chuki dhidi ya Uislamu limejitokeza katika miundo na mifumo mbalimbali rasmi na isiyo rasmi, na kutoa taswira iliyopotoshwa kuhusu Uislamu na Waislamu, sambamba na kuwawekea vikwazo na mashinikizo mengi ya kisaikolojia na kisheria Waislamu wanaoishi Marekani. Baadhi ya viongozi wa Marekani na nchi za Ulaya wamekuwa wakieneza chuki dhidi ya Uislamu na kuchochea ukatili dhidi ya Waislamu. Mfano wa wazi kabisa katika uwanja huo ni Rais Donald Trump wa Marekani ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kueneza na kuchochea chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu wa Marekani na Magharibi kwa ujumla.
Katika mkondo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ameelezea wasiwasi wake juu ya "ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu", akitoa wito kwa serikali kulinda uhuru wa kidini, na kwa majukwaa ya mtandaoni kuzuia matamshi ya chuki.
Vilevile Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Miguel Angel Moratinos, amesema Waislamu wanakabiliwa na "ubaguzi wa kitaasisi na vikwazo vya kijamii na kiuchumi".
Angel Moratinos ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba: "Mienendo hiyo unadhihirika katika unyanyapaa na mienendo ya ubaguzi wa rangi kwa Waislamu na inaimarishwa na vyombo vya habari vyenye upendeleo, matamshi na sera za chuki dhidi ya Uislamu za baadhi ya viongozi wa kisiasa."
Baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023, na mafanikio ya wapigania uhuru wa Palestina katika kukabiliana na mashambulizi ya kinyama na ya kikatili ya jeshi la Israel huko Gaza, vyombo vya habari vyenye uhusiano na Marekani na Magharibi vilifanya juhudi kubwa za kupotoshwa habari na ukweli kuhusu vita vya Gaza.
Maafisa wa Marekani na baadhi ya serikali za nchi Ulaya, pia kwa makusudi, wameanzisha vita vya kipropaganda dhidi ya Wapalestina, kambi ya Muqawama, nchi na shakhsia huru wanaounga mkono na kutetea mapambano ya Wapalestina. Vitendo vilivyopangwa vya kukabiliana na mitandao na vyombo huru vya habari pia ni sehemu ya vita vya kipropaganda vya Wamarekani vya kukabiliana na kambi ya Muqawama, na pia kueneza chuki dhidi ya Uislamu katika maoni ya watu wa Magharibi.
Hata hivyo, njama ya pamoja ya Wamarekani na Wazayuni ya kuchochea chuki dhidi ya Uislamu na Palestina haitafanikiwa na hatimaye itagonga mwamba, kwa kuzingatia harakati kubwa ya waungaji mkono wa Palestina na Muqawama duniani kote, na matumizi yao ya mtandao ya kijamii kwa shabaha ya kufichua na kueleza hali halisi ya matukio ya Asia Magharibi.
342/
Your Comment