16 Machi 2025 - 17:49
Source: Parstoday
Salami: Tishio lolote dhidi ya Iran litakabiliwa na jibu la kuumiza

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kwamba, Iran itatoa jibu la maangamivu kwa tishio lolote iwapo litatekelezwa kivitendo dhidi ya taifa hili.

Meja Jenerali Hossein Salami amesema hayo hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, Iran inafanya kazi kwa uwazi, ikikubali waziwazi kuwajibika kwa matendo yake, iwe ni operesheni za kijeshi au kuunga mkono juhudi za wanamuqawama.

Ameeleza bayana kuwa, Iran haina nafasi yoyote katika kuundwa na kuongoza sera za makundi ya Muqawama ya kieneo, ikiwa ni pamoja na Harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Kamanda Mkuu wa IRGC amesisitiza kuwa, “Sisi si taifa linalofanya kazi kwa usiri. Sisi ni nguvu ya kijeshi inayotambulika na inayoaminika duniani kote. Ikiwa tutashambulia pahala popote au kumuunga mkono mtu yoyote, tutatangaza waziwazi.” 

Meja Jenerali Salami ameashiria operesheni zilizopita, kama vile "Operesheni ya Ahadi ya Kweli" dhidi ya utawala wa Israel, akisisitiza kwamba Iran daima imekuwa ikitangaza wazi na kuwajibikia vitendo vyake, na kamwe haitakataa au kukubali kwa hadaa juu ya operesheni yoyote.

Aidha Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, tishio lolote litakalotekelezwa dhidi ya Iran litakabiliwa na jibu kali, zito na la uharibifu.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha