18 Machi 2025 - 19:39
Tafsiri ya Aya ya Kwanza ya Surat Al-Maidah

Kwa kuwa "Hakika ya Waumini ni ndugu", basi Muislamu anatakiwa kuhakikisha kuwa anatimiza Haki ya ndugu yake Muislamu, na anatetea Haki yake kama Muislamu na kama ndugu yake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA -: Hojjat al-Islam wal-Muslimin, Sheikh Reihan Yasin, Mkufunzi wa Chuo cha al-Mustafa, Dar-es-Salam, Tanzania, amebainisha katika Darsa la Tafsiri ya Qur’an Tukufu maana na makusudio ya ahadi katika Aya Tukufu ya kwanza katika Surat Al-Maidah.

KWA JINA LA MWENYEEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَوْفُوا بِالْعُقُودِ ۚ أُحِلَّتْ لَكُم بَهِيمَةُ الْأَنْعَامِ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ غَيْرَ مُحِلِّي الصَّيْدِ وَأَنتُمْ حُرُمٌ ۗ إِنَّ اللَّهَ يَحْكُمُ مَا يُرِيدُ﴾

Enyi mlio amini! Timizeni ahadi. Mmehalalishiwa wanyama wa mifugo, ila wale mnao tajiwa. Lakini msihalalishe kuwinda nanyi mmo katika Hija. Hakika Mwenyezi Mungu anahukumu apendavyo”.

Tafsiri ya Aya ya Kwanza ya Surat Al-Maidah

Akitafsiri makusudio na muradi wa Aya hii, ameashiria na kufafanua nukta muhimu kama ifuatavyo :

  1. Aya hii inajumuisha ahadi (maagano) yote, na (ahadi) maagano yote ya ki_Mungu na ya Kibinadamu, pamoja na mapatano (au mikataba) ya Kisiasa na Kiuchumi.

  1. Ufafanuzi juu ya aina za mikataba (mafungamano, au maagano au mapatano) kwa mtazamo wa pande zake mbili: Imegawika katika aina tatu: Wakati mwingine ni mkataba baina ya mja na Mola wake, mara nyingine ni mkataba baina ya mtu binafsi na nafsi yake, na wakati mwingine ni baina ya mtu binafsi na wenzake (wanadamu wenzake).

Kwa maana kwamba: Mwenyezi Mungu anawataka Waumini kutimiza ahadi zote hizo, sawa sawa iwe ni ahadi (mkataba) baina ya Mja na Mola wake, au ahadi baina ya Mwanadamu na Mwanadamu Mwenzake (baina Mja na Mja), na wakati mwingine pia ni ahadi baina ya mtu na nafsi yake mwenyewe.

Tafsiri ya Aya ya Kwanza ya Surat Al-Maidah

Hivyo, hii ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuelekea kwa Waja Wake Waumini kwamba watende namna inavyotakiwa kwa mujibu wa imani katika kutekeleza mikataba (au ahadi)  - kwa maana kwamba: Wanatakiwa kuikamilisha mikataba hiyo (au ahadi hizo au mapatano hayo), kuitimiza, na kutoibatilisha au kuipunguza.

Kwa mantiki hiyo, amri hii inajumuisha mikataba (ahadi, mapatano, maagano) baina ya Mja na Mola wake Mlezi, kama vile kujitolea ipasavyo katika kuhakikisha anatimiza kikamilifu uja (na utiifu) wake kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), na kutopunguza katika ahadi au maagano au haki za Mwenyezi Mungu kwa njia yoyote ile, au vile vile kutopunguza katika haki au maagano au ahadi zilizopo baina yake na Mtume (s.a.w.w) kama vile kumtii na kumfuata akiwa kama Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa Walimwengu wote, na vile vile kutopunguza lolote katika maagano au mapatano au mikataba au ahadi zilizopo baina yake na Wazazi wake na Jamaa zake na wanadamu wote kwa ujumla. Mja huyu wa Mwenyezi Mungu anatakiwa kuheshimu ahadi zote hizo na kudumisha mafungamano, na kuhakikisha kuwa hakatishi mafungamano (maagano) hao.

Pia mja anatakiwa kutimiza Haki zote za usuhuba katika utajiri na umasikini, na katika wepesi na dhiki. Ama kuhusiana na maagano au mafungamano yaliyopo baina yake na Mwanadamu mwingine (au watu wengine) ni mikataba ya miamala, kama vile kuuza na kupangisha, na kadhalika, na mikataba (mafungamano au ahadi) ya kutoa kwa kujitolea kama zawadi, na mfano wa hayo, yote hayo anatakiwa kuyatimiza, bali anatakiwa pia kutimiza haki za Waislamu wenzake ambazo Mwenyezi Mungu ameziweka baina yao kwa kauli yake aliposema:

﴿ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ

Hakika ya Waumini ni ndugu

Tafsiri ya Aya ya Kwanza ya Surat Al-Maidah

Na kwa kuwa "Hakika ya Waumini ni ndugu", basi Muislamu anatakiwa kuhakikisha kuwa anatimiza Haki ya ndugu yake Muislamu, na anatetea Haki yake kama Muislamu na kama ndugu yake, Waislamu wote (bila kutizama madhehebu yao) wanapaswa kuwa na ushirikiano baina yao (ndani yao), wanapaswa kuwa maelewano mazuri baina yao, na wahakikishe kuwa wao ni Waislamu, wanaomtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad (s.a.w.w) pasina kufarakana wala kuzozana wala kugombana, kwa sababu kufanya hivyo kutapelekea wao kama Waislamu kupoteza nguvu zao, na kushindwa na kufeli katika mambo yao, na hatimaye kupoteza heshima yao, na hii kwa hakika ni amri ya Mwenyezi Mungu aliposema:

Tafsiri ya Aya ya Kwanza ya Surat Al-Maidah

"Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane (msigombane) mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao subiri".(Al-Anfal: Aya ya 46)

  1. Mwisho, Samahat Sheikh alibainisha na kutoa ufafanuzi juu ya Kanuni ya Kisheria (ya Ki-Fiqh) inayoitwa: "أصالة اللزوم في العقود  / Asili ya Wajibu Katika Mikataba ", na dalili za kuthibitisha kanuni hiyo kutoka ndani ya Qur’an Tukufu, na Sunna (Hadithi Tukufu za Mtume s.a.w.w), na Akili.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha