20 Machi 2025 - 17:29
Source: Parstoday
Kiongozi wa Mapinduzi: Mwaka 1404 ni "Mwaka wa Uwekezaji kwa ajili ya Uzalishaji"

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu uwa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma ujumbe kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1404 hijria shamsia na kuutaja mwaka huu mpya kuwa ni "Mwaka wa Uwekezaji kwa ajili ya Uzalishaji."

Ayatullah Khamenei leo Alhamisi ametuma ujumbe kwa mnasaba wa kuanza mwaka 1404 hijria shamsia na kuashiria kwenda sambamba kuanza mwaka mpya na mikesha ya Laylatul Qadr na kuuawa shahidi Imam Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (AS) na kueleza matarajio yake kwamba: 'Baraka za Laylatul Qadr na mazingatio  ya Bwana wa WachaMungu zitawajumuisha wananchi azizi wa Iran na wale wote ambao mwaka wao mpya unaanza na Nouroz.'

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mwaka 1403 hijria shamsia ulikuwa mwaka uliojaaa matukio mbalimali sawa kabisa  na yale ya muongo wa 60 ulioambatana pia na masaibu na matatizo kwa wananchi na kusema: 'Kuuawa shahidi idadi kadhaa ya washauri wa kijeshi wa Iran huko Syria, kufa shahidi Rais aliyependwa na wananchi Sayyid Ebrahim Raisi na baada ya hapo matukio machungu ya hapa mjini Tehran na huko Lebanon yalilipelekea taifa la Iran na Umma wa Kiislamu kupoteza shaksia wa thamani kubwa mwaka huo.'

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja ugumu wa matatizo ya kiuchumi na masaibu mengine ya maisha khususan katika nusu ya pili ya mwaka huu kuwa ni matukio mengine yaliyoikumba nchi mwaka huu na kusema: 'Katika kukabiliana na matatizo haya; kulijitokeza jambo kubwa na la kushangaza yaani irada thabiti na nguvu ya kimaanawi ya taifa la Iran na utayarifu wa hali ya juu wa nchi hii ambapo dhihirisho lake la kwanza lilihusiana na kumpoteza Rais wa nchi, nara na moyo wa hali ya juu ulioonyeshwa na wananchi katika mazishi makubwa, jambo lililothibitisha kuwa msiba huo mzito haukuweza kuibua hali ya unyonge na udhaifu miongoni mwa wananchi.'

Ayatullah Khamenei ametaja kufanyika uchaguzi wa rais haraka katika muda ulioainishwa kwa mujibu wa sheria na kuiondoa nchi katika ombwe la kusalia bila ya uongozi kwa kumchagua rais na kuunda serikali mpya kuwa ni dhihirisho jingine la ari na uwezo wa juu wa kimaanawi wa Wairani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja sababu nyingine iliyolipelekea taifa la Iran kuwa na nguvu ya kimaanawi kwamba: 'Taifa la Iran lilituma misaada mikubwa ya wananchi kwa ndugu zao wa kidini huko Lebanon na Palestina ili kutatua matatizo ya pande mbili hizo.' 

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake wa Nouroz, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kupewa jina la "Mwaka wa Uzalishaji Mkubwa kwa Kuwashirikisha Wananchi" mwaka wa 1403 hijria shamsia na kusema: 'Matukio ya mwaka uliopita yamekwamisha kutimia kauli mbiu hii licha ya juhudi za serikali, wananchi na sekta binafsi; kwa msingi huo  kauli mbiu na kadhia kuu ya mwaka huu bado ni suala la uchumi na  kuzingatia uwekezaji. Hii ni kwa sababu suala la kuimarisha uzalishaji na kutatua matatizo ya wananchi, linategemea uwekezaji katika uzalishaji.'

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha