Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Khaled Khiari, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya siasa ametoa ripoti kuhusu hali mbaya ya Gaza baada ya Israel kukiuka makubaliano ya kusimamisha mapigano na kubadilishana mateka yaliyoendelea kwa karibu miezi miwili.
"Kadiri siku inavyopita ndivyo tunavyojiweka mbali na lengo la kuwarejesha salama majumbani kwao mateka waliosalia," amesema Khaled Khiari.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuanza tena mazungumzo ya kusitisha mapigano na utoaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza bila vizuizi vyovyote.
Khiari ameashiria matamshi ya Tom Fletcher afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada mapema wiki hii katika kikao cha Baraza la Usalama kwamba "Usitisha mapigano ndiyo njia bora zaidi ya kuwalinda raia wa eneo la Gaza linalokaliwa kwa mabavu na Israel, kuwaachilia mateka na wafungwa na kuruhusu misaada na vifaa vya kibiashara kuingia huko Gaza."
Alkhamisi iliyopita Baraza la Umoja wa Ulaya pia lililaani kukiukwa makubaliano ya kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza ambao umepelekea kuuawa idadi kubwa ya raia wa palestina na kujeruhiwa wengine wengi katika mashambulizi ya Israel.
Baraza la Ulaya pia limetaka kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza na kusema kuwa ipo haja ya kuendelea mbele na awamu ya pili ya utekelezaji wa makubaliano hayo.
Your Comment