Rutte alisema Jumatano, Machi 26, akiwa safarini Warsaw, mji mkuu wa Poland kwamba: "Acha niwe muwazi kabisa. Sasa si wakati wa kufanya mambo ukiwa peke yako; Si kwa Ulaya wala Amerika Kaskazini. Changamoto za usalama duniani ni kubwa mno kwa yeyote kati yetu kukabiliana nazo akiwa peke yake."
Sisitizo la afisa huyo mkuu wa NATO juu ya ukweli kwamba Marekani na Ulaya pekee yazo haziwezi kukabiliana na changamoto za kiusalama duniani linaonyesha kuwa kambi ya Magharibi kwa ujumla haiwezi tena kukabiliana na changamoto za kimataifa kama ilivyokuwa zamani, kutokana na mabadiliko makubwa yanayotokea ulimwenguni, na hasa kufuatia kuibuka kwa madola mapya yenye nguvu kimataifa, hasa China na Russia. Nchi mbili hizi zimesisitiza mara kwa mara nia na azma yao ya kuanzisha na kuendeleza mfumo mpya unaozingatia maslahi ya pande kadhaa duniani na wakati huo huo kupinga sera za upande mmoja za Marekani dhidi ya mataifa mengine. Marais Vladimir Putin wa Russia na Xi Jinping wa China wanachukulia juhudi za kuunda ulimwengu wenye kuzingatia kambi moja ya nguvu duniani kuwa jambo lisilokubalika kabisa.
Hii ni katika hali ambayo, baada ya kuchaguliwa tena Rais Donald Trump wa Marekani, mpasuko unaoendelea kati ya pande mbili za bahari ya Atlantiki kwa mara nyingine unazidi kupanuka, ambapo tofauti kati ya Marekani na Ulaya katika nyanja mbalimbali za kiusalama na kijeshi, kiuchumi na kibiashara na nyinginezo likiwemo suala la mabadiliko ya tabianchi, zinaongezeka kila siku. Katika nyanja ya usalama na kijeshi, suala kuu kati ya Marekani na Ulaya ni ukosoaji wa Trump kuhusu hali ya sasa ya NATO na wanachama wa Ulaya wa shirika hilo la kijeshi pamoja na takwa la kutengwa asilimia 5 ya pato jumla la uzalishaji wa nchi hizo badala ya asilimia 2 kwa ajili ya bajeti zao za kijeshi na kiulinzi. Kwa kuongezea, Trump haamini tena kuendelea Marekani kudhamini usalama wa Ulaya, na hata alisema karibuni kwamba nchi za Ulaya, kinyume na madai yazo, zimetoa pigo kubwa kwa nchi hiyo kuliko maadui zake.
Mbali na masuala hayo, mtazamo wa Trump kuhusu vita vya Ukraine na ulazima wa kuvimaliza haraka iwezekanavyo kupitia mapatano na Russia kumeibua hasira kali miongoni mwa nchi za Ulaya wanachama wa NATO, hasa kwa vile kimsingi Trump amechukua hatua kuhusiana na vita vya Ukraine bila kuzingatia maoni na mitazamo ya nchi za Ulaya ambazo ni wanachama wa NATO, hususan Ujerumani, Ufaransa na Poland. Katika hali ambayo kwa mtazamo wa Ulaya, Russia ni tishio kwa usalama wa nchi za Ulaya, utawala wa Trump umechukua msimamo tofauti kuhusu suala hili na kimsingi unakanusha tishio la usalama kwa Ulaya kutoka Russia. Kwa mantiki hiyo, Februari 2025, J.D. Vance, Makamu wa Rais wa Marekani alisema katika Mkutano wa Usalama wa Munich kwamba, kwa mtazamo wa Marekani, tishio kubwa zaidi kwa usalama wa Ulaya halitokani na Russia wala China, bali linatoka ndani ya Ulaya yenyewe.
Haya yamezipelekea nchi hizo kufikiria namna ya kuunda nguvu yao huru ya kijeshi. Juhudi nyingi za Ulaya bado zinafanyika katika mkondo ule ule wa zamani wa kugawana gharama za mzigo wa usalama. Hatua hizi ni pamoja na kuongeza ushiriki wa Ulaya katika kudumisha ahadi za Marekani za kudhamini usalama wa Ulaya. Ingawa kwa mtazamo wa Marekani inayoongozwa na Trump, licha ya kuwa msimamo huo wa Ulaya uko katika mwelekeo sahihi, lakini bado unapuuza suala la msingi. Kwa hakika, Marekani haitaki kuendelea kuwajibikia usalama wa Ulaya, si kimaadili, kifedha wala kijeshi. Trump anaamini kwamba nchi za Ulaya si tu zinapasa kuchukua majukumu zaidi, bali zinapaswa kujibebea zenyewe mzigo wao wa usalama.
Katika hali ambayo Trump anawashinikiza wanachama wa Umoja wa Ulaya wa muungano wa NATO ili waongeze bajeti yao ya kijeshi, nao Wazungu kuwa na shaka kuhusu kujitolea kwa Marekani kwa shirika hilo la kijeshi, Katibu Mkuu wa NATO bado anajaribu kuanzisha maelewano na maridhiano kati ya pande mbili za Bahari ya Atlantiki. Katika uwanja huo, Mark Rutte amesema kuwa kwa sasa "hakuna mbadala kwa NATO." Na katika hali ambayo nchi za Ulaya zinajaribu kupunguza utegemezi wao kwa Marekani, amesema: "Ulaya inapaswa kujua kwamba Mjomba Sam (Marekani) bado anaiunga mkono, nayo Marekani inapaswa kujua kwamba washirika wake katika NATO wanaimarisha uwezo wao na kutekeleza majukumu yao bila kusita wala kuzembea." Amesema: "Hakuna kitu kinachoweza kuchukua nafasi ya mwavuli wa nyuklia wa Marekani ambao ni mdhamini mkuu wa usalama wetu." Kwa mujibu wa mapatano ya NATO, shambulio dhidi ya mmoja wa wanachama ni sawa na kushambuliwa wanachama wake wote."
Licha ya juhudi za Katibu Mkuu wa NATO, mwelekeo na ukweli unaonyesha kuwa migawanyiko inayoshuhudiwa katika muungano huo wa kijeshi si ya kupita tu, bali itaongezeka katika muhula wa pili wa urais wa Trump. Ni wazi pia kwamba juhudi zinazofanywa na madola pinzani dhidi ya mfumo mmoja wenye nguvu duniani, hasa China na Russia, hatimaye zitadhoofisha pakubwa utawala na udhibiti wa nchi za Magharibi ulimwenguni, kwa kuzingatia kuwa nchi hizo, zikiongozwa na Marekani, hazina tena uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoibuka kila uchao katika ngazi za kimataifa.
342/
Your Comment