Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul - Bayt (a.s) - ABNA -: Mwanaharakati za Kidini, Mtumishi wa Uislamu na Waislamu, Mpenzi na Mfuasi wa Ahlu-Bayt Rasulillah (amani iwe juu yao), Ukthi Fatima Mwiru, ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C), na Mwenyekiti wa Wanawake wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C), ameaga Dunia na kuelekea katika Rehma za Mola wake Mtukufu mapema leo (mchana) Ijumaa (28 Machi, 2025) ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, na ikiwa ndio (Siku ya Quds Duniani) ya kuungana na Waislamu wote kote Duniani katika kutetea na kusapoti wadhulumiwa wa Taifa la Palestina.
Marhuma, Ukthti Fatima Mwiru, Mwana Tabligh, Mtetezi wa Haki, Ukweli na Uadilifu kwa watu wote, miaka yote (mpaka mwisho wa Uhai wake), alikuwa mstari wa mbele katika utumishi bora uliotuka wa kuhudumia Uislamu na Waislamu, na alikuwa ni Kinara Mtetezi wa Haki za Wanyonge na Wadhulumiwa wa Palestina, kwa kupaza Sauti yake katika Jamii ya Wanawake na Watu wote kwa ujumla, katika kuungana na Wanawake na Watoto wa Palestina wanaokumbana na ukandamizaji na mauaji ya Kimbari ya Utawala Haram na hasibu wa Kizayuni.
Kwa Qadar ya Mwenyezi Mungu, leo hii, katika Siku hii adhimu na yenye baraka ya Ijumaa, ametangulia mbele ya Haki, na huu ndio Mwisho Mwema wa Waja Wema wa Mwenyezi Mungu.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema:
قال رسول الله صلى الله عليه وآله: "من مات يوم الجمعة أو ليلة الجمعة رفع الله عنه عذاب القبر"
"Atakayekufa siku ya Ijumaa au Usiku wa Ijumaa, Mwenyezi Mungu atamwondolea adhabu ya kaburini"
Marhuma, Ukthi Fatima Mwiru, Enzi za Uhai wake akiwa katika kutekeleza moja ya Majukumu yake ya Kitabligh
Hadhara ya Uislamu ni Amani Umoja na Mshikamano
Inna Lillah wa Inna Ilayhi Rajiun
Na Mwisho Mwema ni wa Wale Wamchao Mwenyezi Mungu.
Your Comment