3 Aprili 2025 - 18:12
Source: Parstoday
Baraza la Haki la UN lalaani mauaji mapya ya kimbari Gaza

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kulaani mashambulizi mapya ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Baraza hilo pia limeutaka utawala wa Kizayuni "kuzuia mauaji ya halaiki" na "kuondoa mzingiro haramu" kwenye eneo hilo.

Azimio hilo ambalo liliwasilishwa na aghalabu ya wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) lilipasishwa jana Jumatano kwa wingi wa kura. Azimio hilo lilipitishwa na wajumbe 27 kati ya 47 wa baraza hilo ambao walipiga kura ya ndiyo, wanne walipinga na 16 hawakupiga kura.

Wanachama wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa wameeleza kusikitishwa na "ukiukaji wa Israel wa makubaliano ya kusitisha mapigano."

Azimio hilo limeonyesha wasiwasi mkubwa kutokana na matamshi ya maafisa wa Israel ambayo yanaelekea kuchochea mauaji ya kimbari.

Baraza la Haki la UN lalaani mauaji mapya ya kimbari Gaza

Azimio hilo limetaka kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu na mahitaji ya kimsingi huko Gaza pasina kizuizi chochote. Pia limeshutumu utumiaji wa njaa dhidi ya raia kama silaha ya vita.

Kadhalika azimio hilo limetoa wito kwa nchi zote "kuchukua hatua za haraka kuzuia wimbi la Wapalestina kuhamishwa kwa nguvu ndani au kutoka Ukanda wa Gaza."

Aidha limetoa wito kwa mataifa yote kusitisha uuzaji wa silaha kwa Israel na kuchukua hatua za haraka kuzuia kuhamishwa kwa lazima Wapalestina kutoka Gaza.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha