Msafara wa kielimu wa Qur’ani, ukiongozwa na Shaykh Muhammad Mahdi Haqqgouyan — hafidh wa Qur’ani nzima — ulisafiri kuelekea Iraq katika mwezi wa Ramadhani (Machi). Sheikh Haqqgouyan ameeleza kwa IQNA kuwa ujumbe huo ulikuwa na vijana watatu waliokamilisha hifdh ya Qur’ani pamoja na maqarī mashuhuri.
Vipindi hivyo vya Qur’ani vilifanyika katika miji kadhaa ya Iraq, ikiwemo Baghdad na Basra, ndani ya kipindi cha wiki mbili walichokaa nchini humo.
“Kwenye nyanja ya hifdh ya Qur’ani, mmoja wa wanafunzi wangu, Sayyid Ali Murtadhawi, ambaye anafundisha mbinu mbalimbali za kuhifadhi Qur’ani, aliendesha vipindi vyenye mvuto mkubwa na mafanikio makubwa,” amesema Sheikh Haqqgouyan.
Ameongeza kuwa katika upande wa qiraa, kijana Ahmad Reza Askari alitoa qiraa za kukumbukwa na zilizojaa hisia. Vilevile, Sayyid Muhammad Husayni ambaye ni mashuhuri katika qasida, alikuwepo na kutoa mchango wake.
“Watatu hawa ni watu wanaotambulika sana na kuheshimiwa katika fani zao husika,” amebainisha.
Haqgouyan amesema kuwa umati wa watu walionesha hamasa kubwa kwa kushiriki katika mikusanyiko hiyo. “Kwa siku tuliendesha vipindi viwili hadi vitatu, japokuwa mahitaji yalikuwa makubwa zaidi. Kwa bahati mbaya muda haukutosha kuongeza vipindi zaidi. Hamasa hii ilidhihirika zaidi katika vyuo vikuu, ambako idadi kubwa ya wanafunzi na washiriki walihudhuria.”
Aidha, Haqqgouyan amebaini kuwa maafisa wa mkoa wa Basra waliwasilisha ombi la kuanzishwa kwa taasisi ya Qur’ani katika eneo hilo. “Tulikubaliana kuwa suala hilo lichunguzwe kwa kina ili kuona uwezekano wa kuanzisha taasisi hiyo kwa madhumuni ya kutoa elimu na mbinu bora za kuhifadhi Qur’ani Tukufu.”
342/
Your Comment