5 Aprili 2025 - 23:35
Source: Parstoday
Safari ya Netanyahu nchini Hungary na kupuuzwa agizo la ICC la kumkamata mhalifu huyo

Afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orbán ametangaza kuwa nchi hiyo inajitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Tangazo hilo limetolewa saa chache baada ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu kuwasili mjini Budapest.

Netanyahu, ambaye kwa mujibu wa hati iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, anatakiwa akamatwe na kukabidhiwa kwa mahakama hiyo akikabiliwa na tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza, ameamua, huku akiandamana na mkewe, kufanya ziara rasmi ya kuitembelea Hungary ambayo ni nchi mwanachama wa mahakama hiyo.

Safari ya Netanyahu nchini Hungary na kupuuzwa agizo la ICC la kumkamata mhalifu huyo

Hii ni safari ya kwanza kufanywa na Netanyahu barani Ulaya tangu ICC ilipotoa hati ya kutaka akamatwe, mnamo mwezi Novemba mwaka jana. Waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni ameitaja Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuwa ni "mahakama fisadi" na amekaribisha hatua ya Hungary kujiondoa katika mahakama hiyo. Waziri Mkuu wa Hungary alikuwa ameahidi tokea hapo kabla kuwa Budapest haitatekeleza agizo la ICC. Hungary iliidhinisha Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai mwaka 2001, lakini haijawahi kutangaza kwamba inautekeleza rasmi, na kwa hiyo inasema, hailazimiki kutii maamuzi yake.

Kukaidi Hungary kutekeleza agizo la kumkamata Netanyahu, ikiwa ni nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya na ambayo imetia saini Mkataba wa Roma, kumekabiliwa na mijibizo kadhaa kutoka Umoja wa Ulaya. Anita Hipper, msemaji mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ameashiria msimamo wa umoja huo wa kuunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kanuni zilizobainishwa ndani ya Mkataba wa Roma, na akasema: "tunazitaka nchi zote kushirikiana kikamilifu na mahakama hii, ikiwa ni pamoja na kutekeleza haraka hati za utiaji nguvuni". Hipper amekumbusha kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 127 cha Mkataba wa Roma, kujitoa katika Mahakama ya ICC kunawezekana tu kwa taarifa rasmi ya maandishi inayotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa; na kujitoa huko hakutaanza kutekelezwa mpaka upite mwaka mmoja baada ya kutolewa taarifa rasmi. Kutangazwa uwezekano wa nchi kujiondoa katika mahakama ya ICC hakuifutii majukumu inayoendeleai nayo wakati wa kutangaza uamuzi huo ya kutoa ushirikiano kwa mahakama katika mashauri ya kimahakama.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock yeye pia ameizungumzia safari ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni nchini Hungary na kusema: "leo ni 'siku mbaya' kwa sheria za kimataifa".

Erika Guevara-Rosas, mkuu wa kitengo cha utafiti na upangaji sera kimataifa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, amesema katika taarifa: "Netanyahu anatuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Iwapo ataingia katika ardhi ya nchi mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai lazima akamatwe na kukabidhiwa kwa mahakama hii. Mwaliko wa Hungary kwa Netanyahu ni upuuzaji wa wazi kabisa wa uadilifu wa kimataifa na kuwatusi wahanga wa jinai za Ghaza".

Licha ya malalamiko na ukosoaji wote huo, serikali ya Hungary inadai kwamba, maamuzi yaliyotolewa na ICC ni ya kisiasa na ya uingiliaji. Akijibu dai hilo, msemaji wa mahakama hiyo ya kimataifa amefafanua kuwa, nchi wanachama hazina ustahiki wa kuhoji kwa upande mmoja mamlaka ya kisheria ya Mahakama ya ICC. Kulingana na Mkataba wa Roma, nchi ambazo ni wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai zina wajibu wa kutekeleza hati za ukamataji zinazotolewa na mahakama hiyo, na ukiukaji wowote wa utekelezaji wa majukumu hayo unaweza kupelekea kuchunguzwa kisheria na ICC kupitia mfumo wa usimamizi.

Safari ya Netanyahu nchini Hungary na kupuuzwa agizo la ICC la kumkamata mhalifu huyo

Mnamo Novemba 21, 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati ya kukamatwa waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita  Yoav Gallant kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na kutumia njaa (kwa kuwatesa kwa njaa watu wa Ghaza) kama silaha. Hukumu hiyo ya aina yake na ambayo haijawahi kushuhudiwa iliibua hasira na mjibizo mkali wa utawala ghasibu wa Israel hasa kwa kuzingatia kwamba, kabla ya hapo, utawala huo wa Kizayuni ukisaidiwa na Marekani ulikuwa ukijaribu kila mara kuyafanya makundi ya Muqawama wa Palestina hususan Hamas yaonekane kuwa ni magaidi na wahalifu, na wenyewe kujionyesha kuwa ni mhanga wa jinai za makundi hayo. Hata hivyo jinai zisizo na kifani, zilizokithiri na zisizoweza kufichika za Israel dhidi ya Wapalestina madhulumu wa Gaza na mauaji ya kimbari ya makusudi inayofanya dhidi ya wananchi hao, mbali na kutumia silaha ya njaa na kuzuia pia wasifikishiwe misaada ya kibinadamu, na hata kupiga marufuku shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la UNRWA, yote hayo yaliibua wimbi kubwa la kuulaani na kuushutumu utawala huo duniani kote na kutolewa wito wa viongozi wake waandamizi kufunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai; ambapo hatimaye mnamo Mei 2024, Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC aliwaomba majaji wa mahakama hiyo watoe hati ya kukamatwa Netanyahu na Gallant, ombi ambalo mwishowe lilitekelezwa.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha