Juliette Touma, msemaji wa UNRWA, katika taarifa yake ameeleza kuwa zaidi ya wiki sita zimepita tangu Gaza izingirwe kikamilifu na utawala wa Kizayuni, na msaada wote wa kibinadamu muhimu uko hatarini kuisha. Ameonya kuwa bila msaada huo kufikishwa haraka, Ukanda wa Gaza uko kwenye hatari kubwa ya kuingia katika baa la njaa lisilokuwa na kifani.
Touma amesisitiza kuwa watoto wengi wa Kipalestina wanalala njaa, na ametoa wito wa kusitishwa kwa mashambulizi mara moja, kuondolewa kwa mzingiro na kuruhusiwa kupita kwa msaada wa kibinadamu na bidhaa za kibiashara bila vizuizi.
Njia zote za kufikisha misaada Gaza zimefungwa kikamilifu na utawala wa Kizayuni, hali ambayo imefanya janga la kibinadamu kufikia kiwango cha hatari isiyowahi kushuhudiwa. Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa watoto wapatao 60,000 wanakabiliwa na matatizo makubwa ya kiafya kutokana na utapiamlo na njaa kali. Hakuna upatikanaji wa chanjo wala chakula cha kutosha, na hatari ya vifo kutokana na njaa ni ya kweli na ya dharura.
Tangu mashambulizi ya Israel kuanza tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Gaza, zaidi ya watoto 20,000 wa Kipalestina wameuawa — idadi hii ikiwa ni takriban asilimia 40 ya idadi yote ya mashahidi wa Kipalestina katika kipindi hiki — ikionyesha ukatili wa kiwango cha juu unaotekelezwa na wanajeshi wa Israel dhidi ya raia wa Gaza.
Pamoja na onyo na vilio vya jumuiya ya kimataifa, Israel bado inaendeleza sera yake ya kufunga mipaka, jambo linalowafanya watoto na raia wa kawaida wa Kipalestina kufa kwa njaa kama silaha mpya ya kivita.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mashambulizi haya yanahatarisha usalama na uhai wa Wapalestina, hususan watoto. Shirika la UNICEF limeeleza kuwa hali ya watoto wa Gaza ni ya kutisha, na iwapo vikwazo vya misaada havitaondolewa na mashambulizi yasitishwe, basi hali hiyo itazidi kuwa mbaya zaidi.
Utawala wa Kizayuni, baada ya kushindwa kufanikisha malengo yake ya kijeshi Gaza, umeamua kuvunja makubaliano ya usitishaji vita na kuendeleza mzingiro wa kiuchumi, kama njia ya adhabu ya pamoja kwa Wapalestina — jambo linalokiuka Mikataba ya Geneva na sheria zote za kimataifa, na linachukuliwa kama uhalifu wa kivita. Kwa hakika, sera za sasa za Israel dhidi ya Wapalestina ni mfano hai wa "Apathaidi Mamboleo". Kutengwa kwa Wapalestina na haki zao za msingi, kuwalazimisha kuishi kama wafungwa wa pamoja, na juhudi za kuwang’amiza kwa mkakati — yote haya yanafanana na sera za udikteta zilizoshuhudiwa katika historia ya mataifa kandamizi.
Tofauti kuu ni kuwa Israel imefanikiwa kuendelea na sera hizi kwa kupata kinga kupitia msaada wa Marekani na ushawishi wa makundi ya mataifa ya Magharibi, na hivyo kuepuka kuwajibishwa kimataifa.
Aidha, udhaifu wa taasisi za kimataifa katika kukabili uhalifu unaoendelea Gaza umeipa Israel uhalali wa kimya kuendeleza mashambulizi yake. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likikwama mara kwa mara kupitisha maazimio ya kuzuia uhalifu wa Israel kutokana na misimamo ya Marekani.
Ukimya huu wa jumuiya ya kimataifa unaweza kutafsiriwa kama ushirikiano wa kimya na Israel katika uhalifu dhidi ya ubinadamu. Hali hii imechangiwa zaidi na nchi zinazojinadi kuwa mabingwa wa haki za binadamu kama Marekani na Ujerumani ambazo ama zinauzia Israel silaha au kuzuia azimio lolote la kukomesha vita hivyo.
Moja ya hatari kubwa zaidi kwa sasa ni juhudi za Israel za kuifanya hali hii kuwa ya kawaida. Kupitia vyombo vya habari vya Magharibi vinavyoshirikiana na Tel Aviv, wanajaribu kuifanya dunia ichukulie mzingiro wa Gaza, vifo vya watoto na mashambulizi ya kila siku kama jambo la kawaida na lisiloepukika.
Vifo vya watoto wa Gaza leo ni ushahidi hai kwamba dhana ya "haki za binadamu" imegeuzwa kuwa silaha ya kisiasa na mataifa ya Magharibi — inayotumiwa pale tu inapowahusu au kuwanufaisha kisiasa. Edouard Beigbeder, mkurugenzi wa kanda wa UNICEF kwa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, amesema wazi: "Gaza imegeuka kuwa makaburi ya watoto na familia zao."
342/
Your Comment