14 Aprili 2025 - 19:58
Source: Parstoday
Jeshi la Yemen laangusha ndege ya 19 ya kivita ya Marekani

Jeshi la Yemen limetangaza kuangusha tena ndege ya kisasa ya kivita isiyo na rubani aina ya MQ-9 ya Jeshi la Marekani katika anga ya nchi hiyo.

Kitengo cha UAV (ndege zisizo na rubani) cha Majeshi ya Yemen kilitoa taarifa siku ya Jumapili kuthibitisha kuangushwa kwa droni hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo ni jibu kwa uvamizi unaoendelea kufanywa na Marekani dhidi ya Yemen pamoja na mauaji ya kikatili yanayoelekezwa kwa watu wa Yemen.

Gharama ya wastani ya kutengeneza droni moja aina ya MQ-9 inakadiriwa kufikia dola milioni 33 za Marekani, jambo linalomaanisha kuwa Marekani imepata hasara ya zaidi ya dola milioni 600 kutokana na kuangushwa kwa ndege hizo za kisasa nchini Yemen.

Awali, majeshi ya Yemen yalishambulia maeneo muhimu ya Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Katika operesheni hizo, Yemen ilirusha makombora mawili ya balistiki, yakiwemo makombora ya kasi ya juu (hypersonic), kuelekea kituo cha kijeshi cha Israel na Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion.

Taarifa ya Jeshi la Yemen imesema: “Kwa neema ya Mwenyezi Mungu, operesheni zote mbili zimefanikiwa kufanikisha malengo yake, ikiwemo kufungwa kwa Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion kwa takribani saa moja, kusababisha hofu na taharuki miongoni mwa walowezi, na kuwalazimu mamilioni yao kukimbilia kwenye makazi ya dharura."

Yemen imeapa kuendelea na operesheni dhidi ya malengo ya Marekani na Israel hadi utawala katili wa Israel utakapositisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza na uchokozi wa Marekani dhidi ya Yemen utakapomalizika.

Aidha taarifa hiyo imesema:  “Adui wa Kizayuni pamoja na Wamarekani wanapaswa kutambua kuwa Yemen, ikiwa inajumuisha uongozi wake, wananchi wake, na jeshi lake, haitarudi nyuma katika msimamo wao madhubuti wa kuiunga mkono na kuisadia Palestina inayodhulumiwa, wala hawataachana na wajibu wao wa kidini, kimaadili na kibinadamu, bila kujali athari au matokeo yake."

Operesheni hizo za kulipiza kisasi zimefanyika muda mfupi baada ya Marekani kufanya mashambulizi mapya ya anga katika mkoa wa kati wa al-Bayda pamoja na mikoa ya Sa’ada, Hudaydah na Bani Matar. Raia kadhaa waliuawa katika hujuma hiyo ya Marekani.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha