Kauli mbiu ya maonyesho ya mwaka huu ya Tehran ni "Soma kwa Ajili ya Iran," na inaoana na msisitizo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu nafasi ya vitabu katika kuunda utamaduni na jamii. Katika hotuba yake, Spika Ghalibaf amesisitiza umuhimu wa elimu na utamaduni, hasa katika muktadha wa Kiislamu, na kuongeza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea sana utamaduni.
Amesema pia kwamba uchumi unategemea mabadiliko ya kitamaduni, kama vile kukuza utamaduni wa kazi na uzalishaji.
Maonyesho haya, ambayo yanashirikisha wachapisha vitabu 2,363, yanaonyesha vitabu zaidi ya 270,000, sehemu kubwa yake ikiwa inapatikana kidijitali ili kuhakikisha upatikanaji sawa.
Maonyesho ya vitabu ta Tehran pia yanaangazia uhai wa sekta ya uchapishaji ya Iran licha ya changamoto kama vile matatizo ya kiuchumi, ambayo yameathiri sekta ya vitabu hasa mauzo.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu, Abbas Salehi ametilia mkazo nafasi kuu la vitabu katika utamaduni wa Iran kabla na baada ya Uislamu, akieleza kuwa nguvu ya kudumu ya kitamaduni ya Iran imejengwa kwenye urithi wake wa fasihi, hasa kupitia kazi kama Shahnameh. Amesisitiza umuhimu wa kukuza utamaduni wa kusoma na kubadilishana mawazo kama msingi wa maendeleo ya kijamii na ustawi.
Maonyesho haya pia yanazingatia ushirikiano wa kimataifa, kwa kushirikiana na mashirika 50 ya kigeni ambapo mwaka huu Iraq ni mgeni maalumu. Tukio hili pia linaonyesha ubunifu wa kiteknolojia, kama vile jukwaa la kidijitali la usambazaji wa vitabu na mijadala kuhusu teknolojia za kisasa za uchapishaji.
Ili kupandisha juu kiwango cha usomaji vitabu nchini, serikali imeongeza ruzuku ya ununuzi wa vitabu kwa 25%, kwa ajili ya makundi kama walimu na wanafunzi. Maonyesho haya ya siku 10 si tu kuwa ni soko bali pia ni jukwaa la kubadilishana mawazo, yakilenga kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na kifikra wa Iran, ndani na nje ya nchi.
342/
Your Comment