Katika taarifa kwa waandishi wa habari iliyotolewa na Msemaji wa Umoja wa Mataifa jioni ya Jumanne Mei 6 kwa saa za New York, Guterres alitaka pande zote zijizuie kuendesha operesheni za kijeshi.
Katibu Mkuu wa UN amesema dunia haiko tayari kushuhudia mzozo wa kijeshi kati ya India ya Pakistan.
Mapema Jumatatu ya Mei 5, Guterres alionya juu ya mvutano kati ya majirani hao wawili wa eneo la kusini mwa Asia akisema kuwa mvutano wao umefikia kiwango cha juu kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya karibuni.
Amesema ofisi yake iko tayari kusaidiana na serikali hizo mbili kumaliza mvutano kwa njia za kidipolomasia, huku akisisitiza kuwa “jibu la kijeshi si jawabu.”
Guterres amelaani shambulio la kigaidi la tarehe 22 mwezi Aprili huko Pahalgam kwenye eneo la Jammu na Kashmir, lililosababisha vifo vya takribani raia 26, na wengine wengi walijeruhiwa.
“Kulenga raia hakukubaliki –na wale waliohusika na tukio hilo lazima wafikishwe mbele ya sheria kupitia mchakato halali na wa kisheria,” alisema Guterres.
India imefyatua makombora kadhaa ndani ya ardhi ya Pakistan mapema leo alfajiri na kusababisha vifo vya raia wasiopungua 26, katika mashambulizi yanayoweza kuzusha vita baina ya nchi hizo mbili jirani na hasimu wa miaka mingi. India nayo imedai kuwa mizinga ya Pakistan imeua watu 10 katika mpaka wa nchi hizo mbili.
Mamlaka za Pakistan zimesema makombora ya India yalililenga jimbo linalozozaniwa na pande hizo mbili la Kashmir pamoja na mkoa wa mashariki wa Punjab. Moja ya makombora lilimepiga msikiti kwenye mji wa Bahawalpur na kuua mtoto mmoja na kujeruhiwa watu wengine kadhaa.
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif amelaani mashambulizi hayo ya anga na kusema nchi yake inayo haki ya kulipa kisasi kwa hujuma hizo za India alizozitaja kuwa "kitendo cha kivita".
Pakistan imesema imefanikiwa kutungua ndege tano za Jeshi la Anga la India na ndege moja isiyo na rubani katika hatua ya “kujilinda.” Pakistan imesema kwamba ndege za kisasa za Rafale zilizotengenezwa Ufaransa zilikuwa miongoni mwa ndege za kivita zilizoangushwa pamoja na MiG-29 na SU-30.
342/
Your Comment