Chama kidogo cha upinzani nchini Rwanda-chama cha kijani- kimesema leo kwamba kitaipinga hatua ya kuibadilisha katiba, kumruhusu rais Paul Kagame asimame tena kwa mhula wa tatu mwaka 2017. Rais wa chama hicho Frank Habineza aliliambia Shirika la habari la Ufaransa AFP, kwamba katiba ya Rwanda iliyopitishwa 2003 inaruhusu mihula miwili na hivyo haimruhusu Rais Kagame kugombea mhula wa tatu baada ya kuchaguliwa 2003 na tena 2010. Lakini maafisa wamesema bunge litajadili mabadiliko ya katiba kuzingatia kile wapambe wa rais Kagame walichosema ni takwa la umma. Kwa mujibu wa spika wa bunge Danatilla mukabalisa, jumla ya watu milioni mbili wamesaini waraka wakidai Rais Kagame mwenye umri wa miaka 57, aruhusiwe kubakia madarakani kwa mhula wa tatu.