5 Juni 2015 - 19:27
Umoja wa mataifa waitaka Nigeriakuufungulia mashtaka uhalifu wa Boko haram

Mkuu wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa amemtaka rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari kuchunguza ripoti kuhusu uhalifu wa kutisha unaofanywa na kundi la Boko Haram na madai ya dhuluma zinazofanywa na jeshi la nchi hiyo

Mkuu wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa amemtaka rais mpya wa Nigeria Muhammadu Buhari kuchunguza ripoti kuhusu uhalifu wa kutisha unaofanywa na kundi la Boko Haram na madai ya dhuluma zinazofanywa na jeshi la nchi hiyo. Zeid Ra'aad al Hussein akitowa wito huo leo hii amesema ameona madai ya kuuwawa kwa umati wa watu kwa wakati mmoja, ubakaji na ukataji wa viungo vya watoto kunakofanywa na kundi la waasi wa Kiislamu wa itikadi kali Boko Haram ikiwa ni siku moja baada ya miripuko miwili kuuwa zaidi ya watu 30 katika ngome ya kundi hilo kaskazini mashariki ya nchi hiyo. Ameongeza kusema pia kuna ripoti kwamba jeshi la ulinzi la Nigeria limekuwa likiwadhulumu watu wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuwemo kwenye kundi hilo. Buhari ambaye ameapishwa kuwa rais wa Nigeria wiki moja iliyopita amesema jeshi la Nigeria litakuwa na dhima kubwa katika juhudi za kulitokomeza kundi la Boko Haram kwa kushika maeneo yaliyokombolewa kutoka kundi hilo ambayo hivi sasa yako mikononi mwa wanajeshi wa Nigeria.