26 Desemba 2015 - 15:21
Jeneral Qassim Suleiman aongoza Jeshi la Iraq  katika kukomboa mji wa Ramadi + Picha

Jeshi la Iraq likisaidiwa na wanamgambo wa dhehebu la Sunni na Shia chini ya Uongozi wa Jeneral Qassim Suleiman mtaalam wa vita kutoka Iran

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Jeshi la Iraq likisaidiwa na wanamgambo wa dhehebu la Sunni na Shia chini ya Uongozi wa Jeneral Qassim Suleiman mtaalam wa vita kutoka Iran, linakaribia kuutwaa tena mji wa Ramadi baada ya kuwa chini ya himaya ya magaidi wa kundi la Daesh kwa muda mrefu.

Wanajeshi wa Iraq wamepambana na wapiganaji wa mwisho wa kundi la kigaidi la Daesh waliojificha katika mji wa Ramadi, hata hivyo wanajeshi wa Iraq wamekuwa wwakipunguza kasi ya kusonga mbele kutokana na mitego ya mabomu na hofu ya maisha ya raia ambao wanatumiwa na magaidi hao kama ngao.

Mapigano yalipamba moto karibu na makao makuu ya serikali mjini Ramadi, eneo muhimu ambalo ikiwa litakombolewa upya na vikosi vya serikali itakuwa hatua nyingine kubwa katika kuuokomboa mji huo ulioanguka mikononi mwa kundi la kigaidi la Daesh mwezi Mei, kipindi ambacho wanajeshi wa Iraq waliofundishwa na Marekani waliamua kuacha silaha na kukimbia uwanja wa mapambano.

Kwa sasa mji huo unakombolewa na majeshi ya Iraq yaliyopata mafunzo chini ya wataalamu wa vita kutoka Iran ambao wameonyesha mafanikio makubwa katika uwanja wa vita nchii Iraq na Syria.

Mji wa Ramadi umeharibiwa kwa kiasi kikubwa katika miezi kadhaa ya mapigano, na kamanda wa jeshi la Iraq anasema baadhi ya nyumba zilizotegwa mabomu ilibidi ziteguliwe kwa kutumia kifaa cha rimoti ili kuepusha hasara ya vifo au majeruhi ya raia.

Luteni kanali wa jeshi la Iraq amesema wanajeshi wa Iraq wamefika katika kitongoji cha Hoz, karibu mita 500 kutoka kwa ofisi za serikali.

Mkuu wa baraza la mkoa wa Anbar Sabah Karhout anasema idadi kubwa ya mabomu yaliyotegwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh katika mji huo na uwezekano wa raia waliokwama ambao wanatumiwa kama ngao ya binadaamu ndizo sababu za kuchelewesha juhudi za majeshi ya serikali kuingia mjini humo kwa kasi.

Msemaji wa jeshi la muungano unaoongozwa na Marekani, Kanali Steve Warren amesema kundi la kigaidi la Daesh limewaweka wapiganaji karibu 100 katika barabara inaoyelekea katika jengo la ofisi za serikali.

Taarifa zilizotolewa na kundi la kigaidi la Daesh, zilizungumzia idadi kubwa ya majeruhi na vifo miongoni mwa wanajeshi wa serikali ikiwa ni pamoja na katika shambulizi ililosema ilifanya na walipuaji watano wa kujitoa mhanga mapema jana magharibi mwa Ramadi.

Jeshi la Iraq limetoa upande mwingine wa shambulizi hilo, likisema washambuliaji waliuawa na risasi za polisi au mabomu yao waliyoyalipua kabla ya kufika katika eneo walilolenga.

Kwa mujibu wa Warren, ndege za jeshi la muungano ziliangusha mabomu 50 katika ngome za kundi la kigaidi la Daesh Jumatano pekee. Operesheni ya kuukomboa tena mji wa Ramadi ilianza miezi kadhaa iliyopita huku wanajeshi wa Iraq wakifunga barabara za kupitishia vifaa na bidhaa za kutumiwa na kundi la kigaidi la Daesh katika maeneo ya Anbar kabla ya kuanza kuukaribia mji huo taratibu, huku wakiyadhibiti madaraja muhimu, barabara na maeneo mengine.

Viongozi wa Iraq wameilaumu Marekani kwa kuwasaidia magaidi wa Daesh kwa kuwashambulia wanajeshi wa Iraq waliomstari wa mbele wakipambana na magiadi hao.

Mwisho wa habari/ 291