Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Maafisa wa Cyprus wamefahamisha kwamba mtu aliyeiteka nyara ndege ya Misri na kumlazimisha rubani kutuwa nchini Cyprus amekamatwa. Msemaji wa serikali ya Cyprus Nicos Christodoulides ametoa taarifa hiyo bila ya kuweka maelezo zaidi katika mtandao wa Twitter. Mtekaji nyara huyo alijitokeza kutoka kwenye ndege hiyo aina ya Airbus 320 akiwa ameweka mikono yake juu na kujisalimisha kwa polisi wa kupambana na ugaidi katika uwanja wa ndege wa Cyprus. Mtekaji nyara huyo kwa jina Seif Eldin Mustapha alilazwa chini na kukaguliwa kila sehemu kwa muda wa dakika mbili kabla ya kuchukuliwa na polisi hao. Awali mtekaji nyara huyo alidai kwamba amevalia mkanda wa miripuko wakati alipoiteka nyara ndege ya Misri. Hata hivyo inaelezwa hakuna miripuko yoyote iliyokutwa na kwamba mkanda aliokuwa ameuvaa haukuwa wa mabomu. Waziri wa shughuli za usafiri wa anga wa Misri amesema abiria wote na wafanyakazi wa ndege hiyo wako salama. Kwa upande mwingine waziri mkuu wa Misri Sherif Ismail amesema mtekaji nyara ni raia wa Misri aliyekuwa ameomba kukutana na maafisa wa Umoja wa Ulaya au kuielekeza ndege hiyo katika uwanja mwingine wa ndege.
Waziri mkuu Islmail pia amesema mtu huyo atahojiwa kubaini dhamira yake ambayo hadi sasa haifahamiki.
Mwisho wa habari/ 291