7 Novemba 2020 - 09:14
Sisitizo la Putin la kumuunga mkono Lukashenko mkabala na vikwazo vipya vya nchi za Magharibi

Maandamano makubwa yaliyofanyika hivi karibuni nchini Belarus kufuatia uchaguzi uliomrejesha tena madarakani Rais Alexander Lukashenko, kilikuwa kisingizio kizuri kwa nchi za Magharibi kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuanza kutekeleza vikwazo na siasa za uhasama dhidi ya serikali yake.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katika kukaribia kuanza kutekelezwa vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Belarus, ikulu ya Kremlin ilitangaza Jumatano usiku kwamba Rais Vladimir Putin wa Russia amekuwa na mazungumzo ya simu na mwenzake Alexander Lukashenko wa Belarus ambapo wamesisitiza udharura wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Sisitizo la Putin la kumuunga mkono Alexander Lukashenko na serikali yake mkabala na uadui wa nchi za Mgharibi, kwa hakika ni dhihirisho jingine la makabiliano jumla yaliyopo kati ya Russia na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, ambazo zinafanya juhudi za kuidhoofisha serikali ya Moscow na washirika wake. Belarus ambayo ni moja ya washirika wakubwa wa Russia katika miezi ya karibuni imekuwa mlengwa mkuu wa siasa hizo za uhasama za Marekani na washirika wake wa Ulaya. Kufuatia uchaguzi wa karibuni huko Belarus, kumeibuka wimbi la malalamiko  ya uchaguzi na machafuko ambalo bado linaendelea hadi sasa. Wapinzani wa Lukashenko ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi huo wa tarehe 9 Agosti kwa kupata asilimia 80 ya kura zilizopigwa na hivyo kufanikiwa kuingoza nchi hiyo kwa kipindi cha sita mfululizo, katika miezi ya karibuni wamekuwa wakifanya maandamano makubwa huko Minsk, mji mkuu, na miji mingine muhimu ya nchi hiyo wakimtaka ajiuzulu na kuruhusu marekebisho muhimu ya kisiasa yafanyike katika nchi hiyo ya Ulaya Mashariki, wakidai kuwa uchaguzi haukuwa huru wala wa wazi.

Wamagharibi na hasa Marekani na Umoja wa Ulaya, wanawaunga mkono kwa hali na mali wapinzani na hivi karibuni wameimarisha mwenendo wao wa kuingilia masuala ya ndani ya Belarus kupitia mashinikizo ya kisiasa na vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Marekani na Ulaya zimetangaza kwa wakati mmoja kwamba hazimtambui rasmi Lukashenko kuwa rais wa Belarus na wakati huo huo kukosoa vikali muamala wa serikali yake dhidi ya wapinzani. Brussels na Washington zimezidisha siasa zao za kuingilia masuala ya ndani ya Belarus kwa ajili ya kumlazimisha Lukashenko aondoke madarakani na kuweka mahala pake kiongozi kibaraka atakayelinda maslahi yao nchini humo. Siasa hizo zinatekelezwa kupitia mashinikizo ya kisiasa, uungaji mkono kwa wapinzani wa serikali na pia vikwazo tofauti dhidi ya viongozi wa serikali ya Minsk.

Akitahadharisha juu ya matokeo mabaya ya uingiliaji wa nchi za Mgharibi katika masuala ya ndani ya Belarus, Gustav Gersel, mtaalamu wa masuala ya Ulaya Mashariki amesema kwamba suala hilo linaweza kuwa na matokeo mabaya mno kwa Umoja wa Ulaya na vilevile Belarus yenyewe.

Katika hatua ya karibuni kabisa ya mashinikizo ya nchi za Magharibi dhidi ya Belarus, Umoja wa Ulaya umepanga kuanza kutekeleza leo Ijumaa, vikwazo vipya dhidi ya Rais Lukashenko pamoja na viongozi wengine 14 wa serikali yake. Vikwazo hivyo ni pamoja na kufungiwa viongozi hao akaunti zao za benki na vilevile kupigwa marufuku kusafiri katika nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Marekani nayo kwa upande wake zaidi ya mwezi mmoja uliopita iliwaweka viongozi wanane wa serikali ya Belarus katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na serikali ya Washington. Miongoni mwa viongozi hao ni waziri wa mambo ya ndani pamoja na naibu wake, wakuu wa jeshi la polisi na viongozi wa ngazi za juu wa idara za usalama wa ndani. Kwa kutilia maanani siasa haribifu zinazotekelezwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya Belarus, tunapasa kutarajia kwamba katika siku zijazo mvutano mkubwa utaibuka kati ya viongozi wa Minsk na Brussels. Licha ya madai matupu yanayotolewa na Washington kwamba inataka kuimarisha uhusiano wake na Minsk, lakini siasa zake za kushirikiana na Umoja wa Ulaya dhidi ya Belarus zinathibitisha wazi kwamba Marekani inashiriki katika njama kubwa ya kutaka kumng'oa madarakani Rais Lukashenko katika nchi hiyo ya Ulaya Mashariki.

342/