14 Novemba 2020 - 09:51
Makundi ya Libya yafikia mapatano, uchaguzi mkuu kufanyika Disemba 2021

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa makundi hasimu na vyama vya siasa nchini humo vimefikia makubaliano ya kuainisha wakati wa kufanyika chaguzi za Rais na Bunge.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Stephanie Williams amesema kuwa washiriki katika mkutano wa mazungumzo ya kisiasa ya Libya nchini Tunisia wamekubaliana kuwa uchaguzi mkuu nchini humo utafanyika tarehe 24 Disemba mwaka ujao wa 2021. 

Williams amesema kuwa changamoto kubwa kwa sasa ni utekelezaji wa mpango wa Kamati ya Kijeshi wa kuanza kuondoa wapiganaji wa makundi mbalimbali katika eneo la katikati mwa Libya na vilevile mamluki wa nchi za kigeni walioko nchini humo. Stephanie Williams amezitaka nchi zote husika kuheshimu matakwa ya Walibya.

Vilevile washiriki katika mkutano wa amani wa Tunisia wamekubaliana kuanzisha baraza jipya la uongozi wa Libya na kamisheni ya utekelezaji ya kipindi cha mpito.

Mjumbe maalumu wa UN nchini Libya amesema kuwa, Umoja wa Mataifa utatoa msaada wa kiufundi katika uchaguzi mkuu ujao nchini Libya.

Haya yanahesabiwa kuwa matokeo ya kwanza ya mkutano wa amani ya Libya ulioanza Jumatatu iliyopita nchini Tunisia na unatazamiwa kuendelea hadi mwanzoni mwa wiki ijayo. Washiriki katika mkutano huo wanawakilisha makundi 75 ya matabaka mbalimbali ya kisiasa na kijamii ya Libya.

342/