11 Januari 2021 - 10:37
Borrell: Shambulio dhidi ya Kongresi ni ishara ya mpasuko katika jamii ya Marekani

Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema shambulio lililofanywa na wafuasi wa Donald Trump katika jengo la Kongresi ya Marekani linadhihirisha mpasuko uliopo katika jamii ya nchi hiyo ikiwa ni matokeo ya utendaji wa serikali ya Trump na kueleza kuwa: Tukio hilo linapasa kuwaamsha waungaji mkono wa demokrasia.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Josep Borrell ameeleza kuwa ameshtushwa na tukio la Jumatano iliyopita ambapo kundi la wahuni lilishambulia Kongresi ya Marekani ili kuzuia kuthibitisha urais wa Joe Biden. Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya ameeleza kuwa: Jumatano iliyopita tulishuhudia wimbi la matukio yenye kutia wasiwasi ambayo yamekuwa yakijiri katika miaka ya karibuni kimataifa. Amesema matukio hayo yanapasa kuwa tahadhari kwa waungaji mkono wa demokrasia.   

Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa tunapasa kukabiliana na mashambulizo dhidi ya thamani za kidemokrasia na kuzuia migawanyiko katika jamii, si huko Marekani tu bali ulimwenguni kwa ujumla.

Kikao cha Kongresi ya Marekani ambacho kilifanyika Jumatano iliyopita kwa lengo la kupasisha ushindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba 3 huko Marekani kilikabiliwa na shambulio la wafuasi wa Donald Trump katika jengo la Kongresi ya nchi hiyo na kusimama kwa masaa kadhaa. Trump ndiye aliyewachochea wafuasi wake kufanya shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa huko Marekani.

Watu watano waliuawa katika shambulio hilo na wengine kadhaa walijeruhiwa.

Baada ya kupita usiku moja ya ghasia na fujo, hatimaye Kongresi ya Marekani ilipasisha ushindi wa Joe Biden, rais mteule wa nchi hiyo katika uchaguzi wa mwaka jana na kumtangaza kuwa Rais wa 46 wa Marekani.

342/