23 Mei 2025 - 18:39
Source: Parstoday
Umoja wa Ulaya kutazama upya mkataba wa ushirikiano wake na Israel

Kufuatia kushadidi jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel huko Gaza na kuibuliwa mzozo wa kibinadamu usio na mfano wake katika ukanda huo unaozingirwa, Umoja wa Ulaya umeanza kufanyia marekebisho makubwa mapatano ya biashara na ushirikiano kati yake na Israel.

Kaya Callas, Mkuu wa Siasa za Nje za Umoja wa Ulaya, amesema idadi kubwa ya nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, yaani wanachama 17 katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje, wameunga mkono hatua hii ili kuandaa njia ya kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza. Amesema: 'Nchi wanachama zinaona kuwa hali ya Gaza haiwezi kuvumilika tena na tunachotaka hasa ni kuwasaidia watu na kufungua njia kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kuwafikia raia.'

Kasi ya kufanyia marekebisho makubaliano ya Umoja wa Umoja wa Ulaya na Israel, ambao ni msingi wa uhusiano wa kibiashara kati ya pande mbili, imeongezeka tangu Israel ilipokiuka usitishaji vita Machi 18, 2025, na kuanzisha tena mashambulizi yake huko Gaza. Kwa mujibu wa wanadiplomasia, nchi 17 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetaka kufanyiwa marekebisho mkataba huo kwa kuzingatia kifungu kinachosisitiza kuheshimiwa haki za binadamu.

Kwa kuzingatia hayo, Umoja wa Ulaya umetangaza nia yake ya kuchunguza iwapo Israel imekiuka majukumu yake kuhusu haki za binadamu kwa mujibu wa Kifungu cha 2 cha Mkataba wa Ushirikiano wa EU na Israel na hatua zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza au la. Kifungu hiki kinafafanua msingi wa mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia kati ya pande hizo mbili.

Mkataba huo unaojulikana kama "Mkataba wa Ushirikiano Kati ya Umoja wa Ulaya na Israel", ambao ulianza kutekelezwa mnamo mwaka 2000, huainisha mfumo mkuu wa uhusiano wa kiuchumi, kisayansi, kiufundi na kisiasa kati ya pande hizo. Kwa mujibu wa Kifungu cha 2 cha mkataba huo, kuheshimiwa haki za binadamu na kanuni za kidemokrasia linachukuliwa kuwa jambo la lazima kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano. Katika wiki za hivi karibuni na kutokana na kushadidi mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya wakaazi wake wasio na ulinzi hususan wanawake na watoto na pia kuibuliwa baa bandia la njaa, kwa kuzuia kufikishwa shehena za misaada ya kibinadamu katika ukanda huo, mashinikizo ya kimataifa ya kutaka kubadilishwa hali hii mbaya na ya kusikitisha dhidi ya binadamu yamekuwa yakiongezeka. Hii ndio maana wanachama kadhaa wa EU wametaka kutazamwa upya mkataba huu. Maafisa wa Ulaya wanasema kuendelea kuzuiwa misaada ya kibinadamu, kuongezeka mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu na Wapalestina kulazimishwa kuwa wakimbizi katika ardhi yao wenyewe, hasa katika eneo la Rafah, kunakiuka wazi kanuni na misingi ya mkataba huo.

Umoja wa Ulaya kutazama upya mkataba wa ushirikiano wake na Israel

Wakati huo huo, Uingereza imesitisha mazungumzo ya kibiashara na Israel na kuweka vikwazo vipya dhidi ya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Ufaransa pia imesisitiza dhamira yake ya kulitambua taifa la Palestina.

Uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kuyapitia upya mapatano ya ushirikiano na biashara na Israel kutokana na jinai zake dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza, umepingwa na utawala huo ghasibu. Upinzani huo wa Israel ambao umetolewa kama kisingizio cha kuendelea kuwaua watu wa Gaza na kuwatwisha njaa, unapingana wazi na hali halisi ya mambo huko Gaza, hususan kulipuliwa mahema ya wakimbizi na kuwaua kinyama. Kwa maneno mengine, badala ya kupambana na wapiganaji wa Hamas, jeshi la Kizayuni limeamua kuwaua kikatili raia wa kawaida, jambo ambalo ni rahisi zaidi kufanywa na jeshi hilo la watenda jinai.

Msimamo mpya wa Umoja wa Ulaya dhidi ya Israel kutokana na kuendelea mauaji ya halaiki na utumiaji njaa kama silaha pamoja na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza kwa lengo la kuwaangamiza wakazi wa ukanda huo na kuwalazimisha kuondoka Gaza, unaonyesha kuwa kipindi cha uungaji mkono wa pande zote wa nchi za Magharibi kwa Israel kimefikia kikomo. Tel Aviv sasa inazidi kupoteza nguvu zake laini na uwezo wa kushawishi maoni ya umma katika nchi za Magharibi, hasa barani Ulaya na Marekani, kwa shabaha ya kuhalalisha vitendo vyake vya jinai dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza.

Kwa hakika jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza ziko wazi na hazifichiki kiasi kwamba aghalabu ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimechukua msimamo katika uwanja huo kwa kupiga kura ya kuunga mkono kuangaliwa upya mapatano ya ushirikiano na biashara na Israel na wakati huo huo kuchukua hatua ya kivitendo katika kushadidisha mashinikizo dhidi ya Tel Aviv.

Bila shaka suala ambalo haliwezi kupuuzwa ni kwamba, Wamagharibi kimsingi ni waungaji mkono na watetezi wakubwa wa Israel, na hata mwanzoni mwa vita vya Gaza, baadhi ya viongozi wa Ulaya walisafiri kwenda Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa ajili ya kuonyesha mshikamano wao na utawal huo unaochinja wanawake na watoto bila huruma. Wamekuwa waungaji mkono wa hatua za kikatili za utawala huo wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza. Hata sasa, hatua hii ya Umoja wa Ulaya, hasa kwa kuzingatia mahusiano mkubwa yaliopo kati ya utawala huo na baadhi ya nchi za Ulaya ambazo ni wanachama wa umoja huo, kama vile Ujerumani, Hungary, na Jamhuri ya Czech, mara nyingi ni hatua ya kipropaganda na kinafiki tu kwa ajili ya kuwahadaa walimwengu. Aidha katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya, kati ya nchi 27 wanachama wa umoja huo, wanachama wake 10 walipinga kutazamwa upya  mapatano ya ushirikiano na biashara na Israel na hivyo kuonyesha mshikamano wao mkubwa na utawala huo haramu.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha