25 Mei 2025 - 23:12
Source: Parstoday
Mtangazaji maarufu wa Uingereza: Siwezi tena kuikingia kifua Israel

Mtangazaji mmoja maarufu wa televisheni nchini Uingereza ambaye kwa miaka mingi alikuwa ni mtetezi mkubwa wa jinai za utawala ghasibu wa Israel, hivi karibuni amekiri kwamba, hatua za jeshi la Israel huko Ghaza ni mauaji ya kimbari na hazivumiliki tena.

Kwa mujibu wa Sama Al-Akhbariya, mtangazaji huyo maarufu wa Uingereza, Piers Morgan ambaye siku zote alikuwa akitetea jinai za utawala ghasibu wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza na mara kwa mara alikuwa akikataa kulaani hatua za kijinai za waziri mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu huko Ghaza akidai ni hatua za kujihami, sasa amesema, jinai za Israel ni kubwa sana na hawezi tena kuukingia kifua utawala wa Kizayuni.

Piers Morgan alisema hayo hivi karibuni katika mahojiano na mwanaharakati wa vyombo vya habari wa Uingereza na Marekani, Mehdi Hussein akimwambia: "Wewe na mimi tumezungumza kuhusu vita hivi mara nyingi wakati wa mzozo huu wa miaka 75, lakini sijawahi kwenda mbali kama wewe katika kuikosoa Israel. Lakini sasa siwezi tena kupingana na hamu yangu ya kuikosoa Israel."

Alisema: "Kinachotokea Ghaza, kutokana na mauaji ya watoto na raia wa Palestina, ni mauaji ya umati, na Ghaza iko chini ya mzingiro na njaa, mambo ambayo yanafanywa kitaasisi. Mashambulizi ya mabomu ya Israel hayakomi na mamia ya watu wanauawa kila siku; na baraza hili la mawaziri la Israel lenye msimamo mkali linazungumza waziwazi kuhusu mauaji ya kimbari."

Mitazamo ya Piers Morgan katika kuutetea utawala wa Kizayuni wa Israel katika mahojiano yake na Bassem Youssef, mwanaharakati wa vyombo vya habari wa Misri mwenye makazi yake nchini Marekani, ilienea haraka kwenye mitandao ya kijamii wiki chache tu baada ya kuanza vita vya Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023. Mahojiano hayo ya televisheni yalipokea maoni ya mamilioni ya watu katika ulimwengu wa Kiarabu na kimataifa, na Morgan aliyumba na kupigwa mweleka na Bassem Youssef katika mahojiano hayo.

Bassem Youssef, aliidhihaki misimamo ya Morgan akisema: "Jeshi la Israel ndilo pekee ambalo huwaonya raia kabla ya kuwashambulia kwa mabomu. Dhihaka kubwa hii! Kwa mantiki hiyo, kama majeshi ya Russia yatawaonya raia wa Ukraine kabla ya kuwashambulia, je, tutaweza kumpongeza Putin na kumwambia, hapo sasa umefanya jambo la haki umewaonya raia kwanza, sasa uko huru kushambulia nyumba zao?"

Your Comment

You are replying to: .
captcha