Kuhusiana na hili, Shirika la Habari la Reuters limekumbusha sera ya "Utofauti, Usawa na Ushirikishwaji" (DEI), ambayo iliahidiwa kuondoa ubaguzi wa rangi miongoni mwa wafanyakazi wa serikali ya Marekani na kuandika: "Kusahaulika mipango ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi kumeshika kasi tangu kuanza kwa awamu mpya ya urais wa Donald Trump, ambapo jamii ya Marekani inashuhudia wimbi jipya la kusahaulika mipango hiyo, ikiwa ni miaka mitano baada ya kutokea kifo cha Floyd."
Mauaji ya George Floyd mnamo Mei 2020 halikuwa tukio la kupita tu bali lilikuwa moja ya mlolongo mrefu wa unyanyasaji wa rangi unaofanywa na polisi ya Marekani dhidi ya watu weusi. Floyd, kijana mweusi, aliuawa baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kutumia sarafu ghushi na kudidimizwa chini ya goti la Derek Chauvin, afisa wa polisi wa Minneapolis kwa dakika 9 na sekunde 29.
Video ya nyakati hizi za kutisha ilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii na kuikasirisha jamii ya Marekani, kiasi kwamba maneno yake ya mwisho ya, "Siwezi tena kupumua," yakawa nara na nembo ya maandamano ya kimataifa dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini humo.
Ingawa ubaguzi wa rangi umekita mizizi katika historia ya Marekani na wala hilo halikuwa suala geni, lakini kusambazwa video hii na kuonyeshwa ukatili wa polisi wa nchi hiyo dhidi ya kijana huyu mweusi kuliibua maandamano ya umma nchini Marekani, huku mamilioni ya watu wakijiunga na maandamano katika miji na majimbo zaidi ya 2,500 kote Marekani wakipiga nara ya "Black lives matter," yaani maisha ya watu weusi ni muhimu.
Derek Chauvin akimdidimiza George Floyd kwa koti
Wakati huo huo, makampuni makubwa ya kimataifa pia yalijiunga na maandamano hayo ambapo yalitoa taarifa zinazounga mkono harakati za "Black Lives Matter". Kwa mfano, Apple iliahidi kuwekeza katika elimu ya walio wachache, Amazon iliahidi dola milioni mia kadhaa kwa ajili ya kuajiri watu wa rangi tofauti na mamia ya makampuni mengine yakatangaza mipango mbalimbali ya kusaidia kutatua suala la ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Licha ya utawala wa Joe Biden kuahidi kukabiliana na tatizo la ubaguzi wa rangi lakini haukufanya lolote la maana katika uwanja huo hata baada ya kuwa madarakani kwa muda wa miaka minne. Ingawa amri nyingi za kiutendaji zilitolewa kuhusu marekebisho katika jeshi la polisi na kulindwa jamii za wachache, lakini amri hizo ima zilifumbiwa macho au hazikuwa na matokeo yaliyokusudiwa.
Kufuatia kuchaguliwa tena Donald Trump katika uchaguzi wa urais wa Marekani, sera za DEI, ambazo zilikuwa zikihimizwa katika makampuni mengi na taasisi za serikali siku chache baada ya kifo cha Floyd, zilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wahafidhina. Trump na washirika wake waliita DEI kuwa "ubaguzi wa rangi wa kinyumenyume" na kuiakisi kama tishio kwa "ubora wa watu weupe."
Kwa hakika, kufuatia kuchaguliwa tena Trump huko White House, mirenngo ya ubaguzi wa rangi na waupe wanaojiona kuwa bora kuliko watu wa ngozi za rangi nyingine imeimarika tena katika jamii ya Marekani. Trump amekuwa akiwaita maafisa wa polisi wabaguzi wa rangi kuwa "mashujaa" na wakosoaji wa ubaguzi wa rangi kuwa "watoto watundu wa mrengo wa kushoto." Ubaguzi wa rangi huo hauonekani tu kwenye nyanja za kisiasa, bali pia katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kitamaduni na kwenye vyombo vya sheria huko Marekani.
Si tabia za ubaguzi wa polisi zimeshughulikiwa wala mfumo wa mahakama kufanyiwa marekebisho. Pengo la mapato kati ya watu weusi na weupe halijarekebishwa wala kupunguzwa, hata kwenye idara za wafanyakazi wa serikali, ambapo walio wachache bado wananyimwa nafasi muhimu za maamuzi. Kwa maneno mengine ni kuwa, ahadi za marekanisho zilizotolewa na watawala wa Marekani kufuatia mauaji ya George Floyd yalikusudiwa tu kupunguza mashinikizo ya kijamii na sio kurekebisha hali ya ubaguzi wa rangi inayotawala katika jamii ya nchi hiyo.
Kwa hakika, miundo ya ubaguzi wa rangi imefumwa na kukita mizizi katika jamii ya Marekani kiasi kwamba hapaonekani kuwepo na nia ya kweli na ya dhati ya kuifutilia mbali. Watu wa rangi tofauti huko Marekani na hasa weusi, wanakabiliwa kwa miongo mingi na tatizo la ukosefu wa usawa katika pembe zote za nchi. Sasa, miaka mitano baada ya kutokea mauaji ya George Floyd, Marekani kwa mara nyingine tena imeonyesha kwamba njia ya kufikia uadilifu na usawa wa rangi ni suala gumu lenye gharama kubwa mbele ya wafuasi sugu wa ubaguzi wa rangi na mirengo ya wahafidhina.
342/
Your Comment