30 Mei 2025 - 22:17
Source: Parstoday
Ayatullah Khatami: Iran katu haitalegeza msimamo kwa haki yake ya matumizi ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani

Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa, Iran katu haitalegeza msimamo kwa haki yake ya matumizi ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo katika hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran na kusisitiza kwamba, Iran ilirutubisha, inarutubisha na itarutubisha madini ya urani na hakuna kulegeza msimamo katika hili.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesitiza kwamba Iran haitaki kutengeneza bomu la atomiki na kwamba, taifa hili kamwe halitaachana na haki yake ya wazi ya matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Ayatullah Khatami aliashiria misimamo ya hivi karibuni ya viongozi wa Marekani kuhusu haki ya Iran ya kurutubisha madini ya urani na kufafanua kwa kusema: Wasiwasi wa Trump mwaka huu sio Iran kuwa na bomu la atomiki kwani yeye na wenzake wanajua kwamba sisi hatuna bomu la atomiki, si kwa sababu ya kuwaogopa wao, la hasha, bali ni kwa sababu Mwenyezi Mungu na Mtume wametuambia kwamba, hampaswi kumiliki silaha za maangamizi ya umati.

Ayatullah Khatami katika sehemu ya pili ya khutba zake za Swala ya Ijumaa wiki hii hapa mjini Tehran amesema kuwa: Tunaelekea katika kumbukizi ya mwaka wa 36 wa kifo cha Imam Khomeini na mwaka wa 36 wa uongozi wa Ayatullah Imam Khamenei. Tunapaswa kuzingatia misingi ya mapinduzi ya Kiislamju yaliyoongozwa na Ruhullah Khomeini na uongozi wa miaka 36 wa kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Your Comment

You are replying to: .
captcha