30 Mei 2025 - 22:22
Source: Parstoday
Je, utawala wa Trump unataka kubadilisha kisiasa mazingira ya vyuo vikuu vya Marekani?

Kutokana na hali ya mvutano inayoendelea kati ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani na Chuo Kikuu cha Harvard, serikali imetaka kufutwa kwa kandarasi zote za kifedha na chuo hicho.

ABC News imemnukuu afisa mmoja wa ngazi za juu katika serikali ya Marekani akisema: "Idara ya Huduma za Umma katika Ikulu ya White House inatarajiwa kutuma barua kwa mashirika ya shirikisho katika siku zijazo ikiyataka kuweka wazi kandarasi zote na Harvard na kujibu swali la iwapo yanaweza kufuta au kuzihamishia sehemu nyingine."

Mzozo kati ya Harvard na serikali ya Marekani umeongezeka tangu kuanza kwa kipindi kipya cha urais wa Donald Trump. Chimbuko la mzozo huu lilianzia katika muhula wa kwanza wa utawala wa Trump, ambapo mara kwa mara alivishambulia vyuo vikuu kwa tuhuma za kupendelea mrengo wa kushoto na kukandamiza sauti za wahafidhina. Harvard, kama moja ya nembo za wasomi wa kiliberali huko Marekani, ililengwa mara kwa mara katika tweet na hotuba za Trump. 

Maandamano ya wanafunzi wa chuo cha Harvard dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza ni suala ambalo limemkasirisha sanaTrump, ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa utawala huo wa ubaguzi wa rangi.

Kadiri jinai za Israel zilipozidi kuongezeka, wanafunzi wengi wa Chuo Kikuu cha Havard walishiriki katika maandamano na kutoa taarifa za kulaani vitendo vya Israel, huku wengine wakizungumzia waziwazi ubaguzi wa rangi wa utawala huo.

Hali hiyo ilikabiliwa na radiamali kali kutoka kwa waungaji mkono wa Israel huko Marekani, na hivyo kuongeza mashinikizo dhidi ya Harvard na vyuo vikuu vingine huru vya Marekani. Ikulu ya White House imedai kuwa Chuo Kikuu cha Harvard kimezembea katika kukabiliana na vitisho dhidi ya wanachuo wa Kizayuni na kushindwa kuwapa nafasi salama, hivyo utawala wa Trump umetangaza rasmi hivi karibuni kwamba utafutilia mbali mikataba yote ya kifedha iliyosalia na Chuo Kikuu cha Harvard, ikiwa ni pamoja na misaada ya utafiti, vifaa vya elimu na bajeti ya masuala ya kiteknolojia. Hatua hiyo imesitisha msaada wa dola bilioni tatu kwa chuo hicho, ambazo kimsingi hutumika katika miradi ya kielimu na matibabu.

Je, utawala wa Trump unataka kubadilisha kisiasa mazingira ya vyuo vikuu vya Marekani?

Kuhusiana na hili, Alan Garber, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Harvard alisema katika taarifa yenye maneno makali kwamba: "Uamuzi wa serikali wa kupunguza ufadhili ni jaribio la wazi la kuadhibu taasisi huru ya kielimu, na sio hatua ya kulinda usalama wa kundi lolote. Uamuzi huu haudhuru tu chuo kikuu, bali pia miradi ya kielimu ambayo inadhamini mustakabali wa nchi." Alisisitiza kuwa vyuo vikuu havipaswi kufanywa kuwa chombo cha utii wa kisiasa na kuwa Chuo Kikuu cha Harvard kitaendelea kusimama imara mbele ya mashinikizo ya kujaribu kupotosha historia na kudhibiti elimu.

Vitendo vya utawala wa Trump havijaathiri Chuo Kikuu cha Harvard pekee bali pia vyuo vikuu vingine vya Marekani.

Kwa hakika maafisa wa utawala wa Trump wanajaribu moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuvidhibiti vyuo vikuu na kuvizuia kukosoa au kuzungumzia jinai za utawala wa Kizayuni. Kitendo ambacho kinachukuliwa rasmi kuwa zoezi la kujaribu kushinikiza na kudhibiti vyuo vikuu vya Marekani.

Kwa hakika, hatua ya Trump si mjadala wa kisiasa wala kimaadili, bali ni hatua hatari inayotishia mustakabali wa kielimu na uhuru wa vyuo vikuu, jambo ambalo bila shaka linahatarisha hadhi ya kimataifa ya Marekani katika nyanja za sayansi na uvumbuzi.

Kama tunavyoona, kuendelea kwa siasa hizo za mashinikizo za utawala wa Trump kumepeleka nchi za Ulaya kualika vyuo vikuu vya Marekani kama vile Harvard kufungua matawi yao katika nchi hizo. Siku chache zilizopita serikali ya Ujerumani ilipendekeza rasmi kuanzishwa tawi la Chuo Kikuu cha Harvard kwenye ardhi yake ambapo Wolfram Weimer, Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo alisema katika taarifa rasmi kuwa vyuo vikuu lazima viwe huru kufuatilia ukweli.  Alisema Ujerumani inakaribisha ushirikiano na Harvard na kukitaka chuo kikuu hicho kianzishe kituo cha elimu na utafiti barani Ulaya. Je, Marekani itawatoa wahanga wasomi wake kutokana na masuala ya kisiasa?

Utafiti uliofanywa na taasisi nyingi za kielimu, ikiwa ni pamoja na Brookings na Carnegie, unaonyesha kuwa mtazamo wa Trump kwa vyuo vikuu ni wa kutaka kuvidhibiti kisiasa, jambo ambalo linaweza kupelekea kuhamia wasomi wa nchi hiyo katika nchi nyingine na hivyo kupunguza hadhi na itibari ya kielimu  ya Marekani katika ngazi za kimataifa.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha