31 Mei 2025 - 18:37
Source: Parstoday
Iran yalalamika kufuatia matamshi ya kichochezi ya Austria kuhusu mpango wa nyuklia

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemwita Naibu Balozi wa Austria mjini Tehran kulalamikia kile ilichokitaja kuwa ni madai ya “kutowajibika na ya kichochezi” yaliyotolewa na idara ya ujasusi ya ndani ya Austria kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ambao ni wa amani.

Michaela Pacher, aliitwa haraka wizara ya mambo ya nje Ijumaa na Alireza Molaqadimi, Mkuu wa Idara ya Magharibi mwa Ulaya katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.

Katika ripoti yake ya kila mwaka kuhusu vitisho vya kimataifa, iliyotolewa Mei 26, Idara ya Ujasusi ya Ndani ya Austria (DSN) ilidai kuwa Iran inaendelea na juhudi za kutengeneza silaha za nyuklia na inaongeza uwezo wake wa makombora.

Molaqadimi amepinga vikali madai hayo akiyataja kuwa hayana msingi wowote, na akasema yanapingana moja kwa moja na ripoti nyingi za Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA). Amesisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran unazingatia kikamilifu sheria za kimataifa na unatekelezwa kwa mujibu wa  Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Amelaani hatua ya shirika hilo la kijasusi la Austria kutilia shaka malengo ya amani ya mpango wa nyuklia wa Iran bila ushahidi wowote. Kwa msingi huo ameitaka serikali ya Austria kutoa maelezo rasmi kuhusu suala hilo.

Kwa upande wake, mwanadiplomasia huyo wa Austria ameahidi kuwasilisha malalamiko ya Tehran kwa serikali yake.

Mapema Ijumaa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, pia alikosoa vikali ripoti hiyo ya Austria, na kuyataja madai hayo kuwa ya “uongo na yasiyo na msingi,” na akaitaka Vienna kueleza kwa nini imechukua hatua ya kutoa tuhuma hizo dhidi ya Tehran.

Baghaei amesema kuwa ripoti hiyo imelenga tu kuchochea taharuki ya vyombo vya habari dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hivyo “haina uhalali wala si ya kuaminika hata kidogo.”

Madai ya Austria yameibuka wakati Iran na Marekani zikiendelea na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja tangu Aprili, kwa upatanishi  wa Oman, yakilenga kufufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015  yanayojulikana rasmi kama Mpango wa Pamoja wa Kila Mtu wa Utekelezaji (JCPOA).

Your Comment

You are replying to: .
captcha