30 Mei 2025 - 15:52
Mada ya Ijumaa Masjidul Ghadir Kigogo Post: "Hijjah na Athari Zake Katika Malezi (ya Watoto na Jamii)"

Tarehe: Ijumaa, 30 Mei 2025. Mahali: Masjidul Ghadir, Kigogo Post – Dar-es-Salaam, Tanzania. Khatibu wa Swala ya Ijumaa: Maulana Sheikh Hemed Jalala. Mada ya Khutba ya Ijumaa: "Hijjah na Athari Zake Katika Malezi". Khutba hii iliangazia Nafasi ya Hijjah kama Shule ya Malezi ya kina, ikihimiza wazazi na jamii kwa ujumla kutumia mafundisho ya Hijjah kuwalea watoto katika misingi ya Utii, Ucha Mungu, Uvumilivu, Unyenyekevu na Umoja. Pia, iliweka msisitizo wa umuhimu wa Mwezi wa Dhilhijja katika historia ya Uislamu na fadhila za ibada ndani yake.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo hii, tarehe 30 Mei, 2025, Sala ya Ijumaa imesaliwa katika Masjid Ghadir, iliyopo Kogogo Post, Jijini Dar-es-Salam - Tanzania. Khatibu wa Ijumaa alikuwa ni: Maulana Sheikh Hemed Jalala, na Mada ya Ijumaa hii ilikuwa ni: "Hijjah na Athari Zake Katika Malezi". Ufuatao ni Muhtasari wa Khutba ya Ijumaa:

Muhtasari wa Khutba ya Ijumaa

Maulana Sheikh Hemed Jalala aliongoza Swala ya Ijumaa na kutoa khutba iliyoangazia athari chanya za ibada ya Hijjah katika Malezi ya Watoto na Jamii kwa ujumla. Alieleza kuwa Hijjah haibebi tu maana ya ibada ya kimwili, bali pia inabeba mafundisho makubwa ya kiroho na kijamii ambayo yanapaswa kufundishwa kwa watoto na vijana wetu.

Mada ya Ijumaa Masjidul Ghadir Kigogo Post: "Hijjah na Athari Zake Katika Malezi (ya Watoto na Jamii)"

Mafunzo Muhimu Kutoka Hijjah:

  1. Utii kwa Mwenyezi Mungu (SWT):
    Hijjah humfundisha Muumini ( Al-Haj) kuwa Mtiifu kwa Mwenyezi Mungu pasina kuhoji kwa lolote. Hili ni somo muhimu kwa watoto wetu, kuwafundisha kutii amri za Mwenyezi Mungu kwa moyo wote.

  2. Unyenyekevu wa Hali ya Juu:
    Mtu aliye katika vazi la Ihram haruhusiwi kutumia manukato, jambo ambalo linafundisha unyenyekevu wa kweli – tofauti na hali ya kawaida ambapo kutumia manukato uwapo katika Swala, ni jambo la kuongeza thawabu. Hii inabeba falsafa ya unyenyekevu kwa Mahujaji. Funzo hilo tunatoka nalo katika ibada ya Hijjah, na ni muhimu kuwapatia funzo hilo watoto wetu na vijana wetu.

  3. Ucha Mungu (Taq'wa):
    Hijjah ni darasa la Taq'wa (Ucha Mungu). Mahujaji wanarejea majumbani mwao wakiwa wamebeba somo hili adhimu la Ucha Mungu, ambalo nalo linapaswa kuingizwa katika malezi ya watoto wetu.

  4. Uvumilivu na Subira:
    Katika Ibada ya Hijjah, Mahujaji hujifunza subira na utulivu wa hali ya juu – hata pale wanapoumizwa au kuudhiwa. Hili ni funzo muhimu kwa jamii zetu.

  5. Maisha ya Amani, Umoja na Usawa:
    Hijjah hufuta mipaka ya ubaguzi wa rangi, kabila au utaifa. Mahujaji wote huvaa sawa tena nguo zenye rangi moja, hufanya ibada pamoja, na hawabaguliwi au kubaguana kwa misingi ya Madhehebu ya Usunni au Ushia. Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) hakutufundisha Usunni wala Ushia - bali alitufundisha Uislamu unaotuunganisha.


Matukio Muhimu ya Mwezi wa Dhilhijja:

Katika sehemu muhimu iliyoashiriwa katika khutba hiyo ni pamoja na Matukio Muhimu ya Mwezi wa Dhilhijja. Maulana Sheikh Hemed Jalala alikumbusha juu ya matukio muhimu ndani ya Mwezi wa Dhilhijja, kwamba Mwezi huu ni Mwezi Mtukufu uliojaa historia na fadhila mbalimbali, na ukiwa na matukio kadhaa yaliyojiri ndani yake kama ifuatavyo:

  • a) Ndoa ya Bibi Fatima (sa) na Imam Ali bin Abi Talib (as).

  • b) Shahada ya Imam Muhammad Al-Baqir (as).

  • c) Kusafiri kwa Imam Hussein (as) kutoka Makka kuelekea Karbala.

  • d) Shahada ya Muslim bin Aqil (ra), Balozi wa Imam Hussein (as).

  • e) Tarehe 18 Dhilhijja – Tukio la Ghadir Khum, kutangazwa kwa Imam Ali (as) kuwa Khalifa moja kwa moja baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w).

  • f) Tarehe 24 Dhilhijja – Siku ya Mubahala.

Maulana Sheikh Jalala alihimiza Waumini kujitahidi kufanya ibada kwa wingi katika siku hizi tukufu za Mwezi huu wa Dhilhijja, kwani fadhila za Masiku ya Dhilhijja ni kubwa mno. Alielekeza kwa Waumini kurejea Mafatihul Jinan kwa mwongozo wa ibada na amali maalum za Mwezi huu.


Mwisho:
Khutba hii iliangazia Nafasi ya Hijjah kama Shule ya Malezi ya kina, ikihimiza wazazi na jamii kwa ujumla kutumia mafundisho ya Hijjah kuwalea watoto katika misingi ya Utii, Ucha Mungu, Uvumilivu, Unyenyekevu na Umoja. Pia, iliweka msisitizo wa umuhimu wa Mwezi wa Dhilhijja katika historia ya Uislamu na fadhila za ibada ndani yake.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha