Katika taarifa rasmi iliyotumwa kupitia shirika la habari la serikali, Saba, siku ya Jumapili, al-Mashat ameonya kuwa mazingira katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel yanazidi kuwa hatarishi kutokana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani (drone) yanayofanywa na Jeshi la Yemen kama sehemu ya kisasi dhidi ya kampeni inayoendelea ya mauaji ya kimbari inayotekelezwa na Tel Aviv katika Ukanda wa Gaza.
Al-Mashat amesema:"Makampuni yote yanayofanya kazi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu lazima yachukulie onyo hili kwa uzito mkubwa, na kuondoka mara moja kabla hali haijawa mbaya zaidi."
Ameongeza kuwa kampuni yoyote itakayopuza onyo hilo italazimika kubeba dhima kamili ya uamuzi wake, pamoja na hasara zitakazotokana na uwekezaji katika mazingira ya hatari.
"Tunaweza kuchukua hatua zaidi katika siku chache zijazo endapo hali itahitaji, jambo ambalo litaweka makampuni haya katika hatari kubwa isiyo na kifani," ameonya.
Al-Mashat pia ameeleza kuwa kupuuza onyo la Yemen ni sawa na "kuwekeza kwenye mazingira ya mtafaruku, jambo ambalo linaweza kuzaa matokeo yasiyopendeza."
Kiongozi huyo wa ngazi ya juu hakusita kukosoa vikali utawala wa haramu wa Israel, akisema: "Serikali ya uhalifu ya Benjamin Netanyahu haijali maslahi ya wawekezaji. Inachezea usalama wao kwa minajili ya ajenda zake binafsi. Utawala usiojali hatima ya mateka wake walioko Gaza hauwezi kulinda makampuni ya kigeni wala mitaji yao."
Aidha, amesisitiza kuwa Jeshi la Yemen litaweka muda maalum kwa makampuni hayo kuondoka katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu, ili kupunguza madhara na kuepuka uharibifu usio wa lazima.
Al-Mashat pia ameonya kuwa athari za mashambulizi hayo huenda zisibaki tu ndani ya maeneo yanayokaliwa, bali zikaenea hadi kwenye mali na vitega uchumi vya nje endapo Yemen itaamua kuongeza kiwango cha mashambulizi yake.
Katika kujibu uvamizi unaoendelea dhidi ya Gaza, Yemen imetekeleza mzingiro wa kimkakati dhidi ya njia muhimu za baharini, kwa lengo la kuzuia usafirishaji wa silaha kwenda Israel na kushinikiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kuhusu janga la kibinadamu linaloendelea Gaza.
Jeshi la Yemen limetangaza bayana kuwa halitasitisha mashambulizi yake hadi pale Israel itakaposimamisha mashambulizi yake ya nchi kavu na anga dhidi ya Wapalestina.
Your Comment