5 Juni 2025 - 15:58
Source: Parstoday
Kwa nini Trump ameshindwa kutatua migogoro ya kimataifa licha ya ahadi zote alizotoa?

Katika makala yake iliyopitia miezi minne ya kwanza ya utawala wa pili wa Donald Trump, tovuti ya CNN imeandika kwamba kabla ya kuingia madarakani, rais huyo alijigamba kwamba alikuwa na uwezo wa kutatua matatizo na migogoro mikubwa ya dunia, lakini hali ya sasa sio nzuri hata kidogo, ingawa yeye si rais pekee wa Marekani kutoa ahadi za uongo kuhusu suala hilo.

Kwa mujibu wa mtandao huu, kila rais wa Marekani anayefika Ikulu ya White House huwa anadhani kwamba anaweza kubadilisha ulimwengu, ambapo Trump amekuwa akihisi hivyo kuliko rais mwingine yeyote wa Marekani. Ni wazi kuwa mambo hayamwendei sawa rais huyo wa 47 wa Marekani. Ingawa Trump anaweza kuwatisha wakuu wa mashirika ya kiteknolojia kufuata maamrisho yake na kutumia uwezo wa serikali kukandamiza vyuo vikuu vya nchi hiyo kama vile Harvard, lakini ni wazi kuwa hawezi kuwatisha viongozi wote wa nchi nyingine za dunia na kuwalazimisha wafanye anavyotaka yeye.

Kukiri kwa chombo hiki cha habari cha Marekani kuhusu kushindwa Trump kumaliza migogoro ya kikanda na kimataifa kwa mara nyingine tena kumefichua utambulisho wake halisi na jaribio lake la kujaribu kuwasilisha taswira bandia kuwa Marekani, ina nguvu, ushawishi na uwezo wa kubadilisha tabia na sera za nchi nyingine ulimwenguni.

Trump, huku akifumbia macho ukweli wa kudhoofika hadhi ya Marekani duniani na kuporomoka kwa uwezo wake, amefanya jitihada zisizo na faida za kuwatisha na kuwashawishi wapinzani wa Marekani na hata washirika wake ili wayakubali matakwa yake na kufungamana na malengo na sera za Washington, lakini bila mafanikio yoyote.

Kwa mujibu wa CNN, miezi minne ya kwanza ya urais wa Trump imethibitisha kwamba licha ya vitisho vya kupandisha ushuru kwa biadhaa za mataifa mengine, maonyo kwa Canada na Greenland ili zijiunge na marekani na kufutwa kimataifa misaada ya kibinadamu ya nchi hiyo, lakini nchi nyingine za dunia pia zina haki ya kutoa maoni kuhusu matukio yanayotokea katika pembe tofauti za dunia. Ni wazi kuwa viongozi wa China, Russia, Ulaya na Canada wametambua kwa sasa kwamba Trump hana nguvu kama anavyodai na kuwa hakuna gharama ya kumkaidi.

Kwa nini Trump ameshindwa kutatua migogoro ya kimataifa licha ya ahadi zote alizotoa?

Rais Xi Jinping wa China (kushoto) na Trump

Kwa hakika juhudi za Trump katika maeneo mbalimbali, hususan kampeni yake ya kuongeza ushuru dhidi ya bidhaa za nchi nyingine, si tu kwamba hazijakuwa na matokeo aliyoyakusudia, bali pia zimeibua hisia kali kutoka kwa washirika wakuu wa kibiashara wa Marekani, hasa China na Umoja wa Ulaya. CNN imeandika kuhusiana na hili kwamba: 'Trump alidhani anaweza kubadilisha siasa za Rais Xi Jinping wa China na kumfanya aendane na matakwa yake katika vita vya kibiashara, lakini haelewi vizuri siasa za China na amekuwa akifanya makosa kuhusiana na suala hilo.' Rais huyo wa Marekani hata amelazimika kulegeza msimamo katika vita vya kibiashara na Ulaya.

Ahadi nyingine tupu ya Donald Trump ilikuwa ni kumaliza haraka vita nchini Ukraine. Kabla ya kurejea Ikulu ya Marekani, aliahidi kwamba angesimamisha vita kati ya Russia na Ukraine ndani ya saa 24. Alidai kwamba kama angebakia madarakani, vita hivi havingetokea kabisa. Sasa, miezi minne baada ya kutawazwa kwake, ahadi hii bado inaonekana kuwa mbali kutimizwa. Sio tu kwamba ameshindwa kumaliza vita hivyo bali kwa kukata msaada wa Marekani kwa Ukraine ameibua mpasuko kati ya White House na washirika wake wa Ulaya. Kwa upande mwingine, Trump ameshindwa kuishawishi Russia isimamishe vita na Ukraine.

Trump pia ameshindwa wazi kuhusu vita vya Gaza. Alimshawishi Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel akubali kusitisha mapigano kwa muda hadi baada ya kuapishwa kwake Januari 20 mwaka huu, lakini muda mfupi baadaye akatoa idhini ya kutumwa silaha za maangamizi kwa utawala huo ili uendeleze mauji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wasio na hatia huko Gaza. Hivi sasa Steve Whitkoff, mjumbe maalumu wa Trump katika eneo la Mashariki ya Kati anajaribu kusimamisha vita vya umwagaji damu huko Gaza, kwa njia ambayo inawiana zaidi na malengo ya utawala wa Kizayuni hususan kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni bila ya kupata hakikisho lolote kutoka kwa Israel kuhusu usitishaji vita wa kudumu. Wakati huo huo, Netanyahu amepuuzilia mbali matakwa ya kimataifa ya kusitisha umwagaji damu Gaza na kuanzisha usitishaji vita wa kudumu.

Matukio haya yote yanaonyesha wazi kwamba Trump anajaribu kujidhihirisha tu kama rais aliye na nguvu kubwa ambaye kila mtu anapasa kumtii, kupitia sera yake ya eti "amani kupitia nguvu," huku akighafilika na ukweli kwamba nguvu laini ya ushawishi wa Marekani katika ngazi za kimataifa imepungua na kudhoofika sana, ambapo anaendelea kuchukiwa kimataifa siku baada ya siku.

Your Comment

You are replying to: .
captcha