Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Donald Trump ameamuru uchunguzi ufanyike kuhusu utendaji kazi wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden wakati wa uongozi wake na kudai kuwa washauri wakuu wa Biden walificha kwamba rais huyo hakuwa na akili timamu.
Joe Biden, ambaye alimshinda Trump katika uchaguzi wa 2020, alijiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais baada ya kumalizika kipindi chake cha kwanza kutokana na kuvurunda vibaya katika mdahalo wa uchaguzi mwaka jana na wasiwasi ukaoongezeka kuhusu uwezo wake wa kiakili.
Uwezo wa kiakili wa Biden uligeuzwa kuwa shabaha ya mashambulizi ya chama cha Trump cha Republican kwa miaka mingi wakati wa urais wake, lakini ripoti katika vyombo mbalimbali vya habari vya Marekani na kitabu cha hivi karibuni kilichoandikwa na mtangazaji wa CNN Jake Tapper kinaonesha kuwa hata maafisa wakuu wa chama cha Democratic na wale wa karibu wa Biden walikuwa na mashaka makubwa juu ya uwezo wake wa kutekeleza majukumu ya urais.
Katika memo, Trump alihoji iwapo Biden alisaini mwenyewe na kwa akili timamu msamaha na hati nyingine au la. Trump amehoji pia matumizi ya Biden ya kifaa cha mitambo cha kutoa saini halisi ambazo marais wa Marekani wamekuwa wakikitumia kwa miaka mingi.
Trump amekuwa akidai mara kwa mara kwamba baadhi ya vitendo vya Biden havina uhalali wa kisheria kwa sababu anasema, washauri wa Biden walichukua wao maamuzi ili kuficha kushuka uwezo wa kiakili wa Biden.
"Kula njama kama hii ni moja ya kashfa hatari na za kutatanisha katika historia ya Marekani," ameandika Trump. "Wananchi wa Marekani walizuiliwa kwa makusudi kujua ni nani aliyeshikilia nafasi kuu ya utawala wa nchi wakati saini ya Biden ilipotumiwa kusukuma maelfu ya hati na mabadiliko ya sera kali (bila ya Biden kujitambua)."
Trump ametoa amri kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Pam Bundy, na Wakili wa Ikulu, David Warrington, kuongoza uchunguzi huo.
Your Comment