Taarifa ya pamoja iliyochapishwa kwenye tovuti ya serikali ya Canada inasema: 'Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kundi la Saba, linalojumuisha Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japani, Uingereza, Marekani na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, walikutana mjini The Hague, Uholanzi, Juni 25, 2025, na kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi.
Katika taarifa hiyo, mawaziri hao wamesisitiza uungaji mkono wao kwa usitishaji vita, wakidai kwamba "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipasi kamwe kupata silaha ya nyuklia," na wakatoa wito kwa Iran kujiepusha kufufua kile walichokitaja kuwa shughuli zisizohalalishwa za kurutubisha madini ya urani. Hii ni licha ya ukweli kwamba Iran siku zote imekuwa ikikanusha madai ya kutaka kuunda silaha za nyuklia.
G7 imeitaka Iran kuendelea kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kusisitiza kwamba Iran lazima itoe taarifa zinazoweza kuthibitishwa kuhusu nyenzo zake zote za nyuklia na kutoa fursa kwa wakaguzi wa shirika hilo wafanye uchunguzi katika vituo vyake vya nyuklia.
Nukta muhimu katika taarifa ya kundi hilo ni kunyamazia kimya hujuma ya kichokozi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, ambapo vituo vya nyuklia vya amani vya Iran vilivyoko chini ya usimamizi wa wakala wa IAEA vililengwa.
Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesema katika mahojiano na CBS kuhusiana na madai ya Donald Trump kwamba mazungumzo yanaweza kurejea wiki hii, kwamba: "Mazungumzo hayatarejea hivi karibuni."
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7
Araqchi ameongeza kuwa: "Ili kuamua kurejea kwenye mazungumzo, ni lazima kwanza tuhakikishe kwamba Marekani haitalenga tena Iran kwa mashambulizi ya kijeshi wakati wa mazungumzo. Kwa kuzingatia mambo haya, bado tunahitaji muda zaidi."
Huku akisisitiza kwamba "teknolojia na ujuzi wa kurutubisha urani hautaharibiwa kwa mabomu," Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, "mpango wa nyuklia wa amani wa Iran umekuwa nembo ya heshima na fahari ya taifa."
Araghchi pia amesema katika kujibu madai ya Marekani kuhusu "kuharibiwa kabisa" vituo vya nyuklia vya Iran kwamba: "Hakuna mtu anayeweza kuharibu ujuzi wa kurutubisha madini na teknolojia kwa mashambulizi ya kijeshi. Ikiwa tutakuwa na nia, na bila shaka kuna nia hiyo, ya kufikia ustawi katika sekta hii kwa mara nyingine tena, tutaweza kufidia haraka hasara na wakati uliopotea."
Hivi sasa, Iran haina nia ya kuendelea na mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani. Msimamo huu unatokana na sababu kadhaa muhimu: Iran inaamini kwamba Washington inatumia mazungumzo si kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo, bali kama njia ya kuongeza mashinikizo dhidi ya Tehran.
Hata katika mazungumzo ya hivi karibuni yasiyo ya moja kwa moja, Marekani imeongeza vikwazo na kuchukua hatua za kijeshi, na hivyo kupelekea Tehran kufikia natija kwamba mazungumzo katika mazingira ya sasa yanatoa fursa kwa upande mmoja pekee.
Iran haiko tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Marekani hadi pale nchi hiyo itakapothibitisha kivitendo kuwa iko tayari kubadilisha tabia zake, ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo na kuachana na vitendo vya kuvuruga usalama wa Iran.
Mazungumzo yoyote ya siku za usoni kati ya Iran na Marekani huenda yakafanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kama kutokuwepo na mikakati ya kuhakikisha kuwa mambo yanayofikiwa yanatekelezwa kivitendo na bila kukiukwa kwa njia yoyote ile. Washington na washirika wake lazima kwanza waheshimu ahadi walizotoa huko nyuma kama vile kufuta vikwazo na kutoa hakikisho la kutokaririwa vitendo vya kichokozi kama vile mashambulizi kwenye vituo vya amani vya nyuklia vya Iran.
Msimamo wa hivi sasa wa Tehran unaonyesha kuwa bila ya kuwepo mabadiliko yaliyoashiriwa katika siasa za Marekani na kutolewa hakikisho la kivitendo katika uwanja huo, Iran haitarejea kwenye meza ya mazungumzo ya nyuklia. Tehran itajiepusha kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani hadi pale mazingira ya kujenga uaminifu yatakapoandaliwa, la sivyo itazingatia tu chaguo la mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja.
Your Comment