Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul Bayt (a.s.) - ABNA - jeshi la utawala wa Kizayuni lilichukua udhibiti wa zaidi ya meli na boti 40 zinazoshiriki katika kampeni ya kimataifa ya msafara wa Al-Sumud siku ya Alhamisi.
Mamia ya wanaharakati waliokuwa katika msafara huo wamehamishiwa bandari ya Ashdod ili kuanza taratibu za kuwafukuza kutoka maeneo yanayokaliwa.
Pia ilitangazwa kuwa boti nne za msafara huo zilishindwa kuendelea na safari kutokana na matatizo ya kiufundi baharini.
Jeshi la Israel limeanzisha operesheni kubwa katika maji yanayozunguka Gaza ili kuzuia boti yoyote isikaribie pwani ya eneo hilo.
Wakati huo huo, waandaaji wa msafara wa Al-Sumud walitangaza kuwa meli "Mikino", mojawapo ya vyombo vya kampeni hiyo ya kimataifa, ilifanikiwa kuvuka vizuizi vya baharini vya Israel na kuingia katika maji ya ardhi ya Palestina mapema Alhamisi. Data za urambazaji za meli hiyo zinaonyesha kuwa iko umbali wa maili 9 za baharini kutoka pwani ya Gaza.
Yousef Ajissa, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Kuvunja Mzingiro wa Gaza, alitangaza kuwa vikosi vya Israel hadi sasa vimekama takriban meli 20 kati ya jumla ya meli 45.
Aliongeza kuwa Israel ilizingatia kukamata meli kubwa na zile za amri ili kuvuruga mwendo wa msafara huo, lakini meli zingine zinaendelea na safari yao.
Ajissa alizitaka serikali na taasisi za kimataifa kuingilia kati ili kulinda afya ya wanaharakati waliokamatwa na kudai kuachiliwa kwao mara moja na bila masharti.
Ni muhimu kutaja kwamba Jeshi la Wanamaji la Israel lilishambulia msafara wa Al-Sumud katika maji ya kimataifa Jumatano jioni na kulilazimisha kuelekea bandari ya Ashdod. Hadi sasa, meli 13 za msafara huo zimekamatwa na makumi ya wanaharakati waliokuwemo wamekamatwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel pia ilitangaza kuwa wanaharakati wa msafara huo wako njiani kuhamishiwa Israel na mchakato wa kuwafukuza kwenda Ulaya utaanza.
Msafara wa Al-Sumud, ulioanza safari yake kutoka Uhispania mwishoni mwa Agosti, unajumuisha meli 45 zinazobeba mamia ya wanaharakati kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.
Your Comment