Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, kufikia mwaka 2045, huenda wanandoa wengi wakahitaji msaada wa teknolojia za uzazi ili kupata watoto. Kauli hii ya Dkt. Shanna Swan si onyo la kitabibu tu; ni kengele ya hatari kutoka kwenye kina cha mgogoro wa utambulisho wa binadamu.
Tatizo haliko tu kwenye kupungua kwa mbegu za kiume, bali kwenye kupungua kwa maana ya kuwa mwanaume - wanaume wasioweza tena kuelewa kwa nini wapo, na wanawake waliochoka kubeba majukumu ambayo hayakuwa yao.
“Qiwāmah” - Neno Lililosahaulika
Katika utamaduni wetu, dhana ya qiwāmah (uongozi wa Mwanaume wa familia) ilipaswa kumaanisha uwajibikaji wa mwanaume katika kujenga, kulinda na kusimama imara, lakini imepotoshwa na kutafsiriwa kama ubabe na ubaguzi. Matokeo yake ni kwamba wanaume wamejiondoa katika majukumu yao, na wanawake wamelazimika kubeba majukumu mawili kwa wakati mmoja.
Mwili, Lugha ya Kimya ya Maana
Wakati uanaume unapoteza maana, mwili wenyewe hutoa ishara. Kupungua kwa testosterone, kushuka kwa kiwango cha mbegu za kiume, na mgogoro wa uzazi - vyote hivi si tu matatizo ya mwili, bali ni dalili za kukatika kwa mishipa ya dhamira. Mwanaume asiyefahamu kwa nini asimame, taratibu hupoteza nguvu ya kusimama.
Wanawake Wenye Nguvu, Wanaume Waliopotea?
Katika hali hii, wanawake wamekuwa na nguvu zaidi - lakini si lazima kuwa na furaha zaidi. Wamekuwa kama wanaume waliowahi kutamani kuwa nao, na wanaume wamegeuka kuwa vivuli visivyo na sauti katika uwanja wa maisha. Huu si usalama wa kijinsia (usawa) wala ustawi - huu ni uchovu wa kijamii.
Mwisho wa Dunia, Maana ya Kupotea kwa Nafasi
Wakati nafasi za kijinsia zinapovunjika, jamii huingia kwenye kipindi cha kuporomoka. Si kwa vita na damu, bali kwa uchakavu wa taratibu wa maana. Huu ndio mwisho wa dunia wa kweli - pale ambapo mwanamume na mwanamke wote wawili hawajui tena kwa nini wapo, na kwa ajili ya nini wanapaswa kuwepo.
Njia ya Kurudi, Ndiyo Njia ya Kusonga Mbele
Tunapaswa kurejelea upya maana ya qiwāmah - si kama mamlaka, bali kama uwajibikaji. Wanaume wanapaswa kujifunza tena kuwa nguzo za jamii, na wanawake waweze kuchanua chini ya kivuli cha ulinzi na msaada huo. Hapo ndipo haki ya kijinsia ya kweli inapopatikana: si kwa kufanana, bali kwa kushirikiana.
Makala hii ni mwaliko wa kurejesha maana - kujenga upya ulimwengu ambao ndani yake, kuwa mwanaume na kuwa mwanamke, vyote vinamaanisha kuwa binadamu kamili, wenye wajibu, maana, na matumaini.
Your Comment