Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Yaoundé, Cameroon - Baraza la Katiba la Cameroon limemtangaza Rais aliyeko madarakani, Paul Biya, kuwa mshindi wa Uchaguzi wa Urais uliofanyika Oktoba 12, na hivyo kumpa muhula wa nane wa uongozi, unaoendeleza utawala wake wa muda wa zaidi ya miaka 43.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na Baraza hilo, Rais Biya ameshinda kwa kupata asilimia 53 ya kura zote zilizopigwa, huku mpinzani wake mkuu, Issa Tchiroma Bakary,

akipinga matokeo hayo na kudai kuwepo kwa udanganyifu wa kura.
Tangazo hilo limekuja baada ya siku kadhaa za mvutano na maandamano makali yaliyosababisha vifo vya takribani watu wanne, hasa katika maeneo ya miji mikuu na ngome za upinzani.
Wafuasi wa upinzani wameishutumu mamlaka kwa “kuiba kura” na wanasisitiza kutambuliwa kwa Bakary kama mshindi halali wa uchaguzi huo.
Akiwa na umri wa miaka 92, Paul Biya sasa ndiye kiongozi mwenye umri mkubwa zaidi duniani aliye madarakani, na iwapo atamaliza muhula wake mpya, anaweza kuendelea kutawala hadi atakapofikisha takribani miaka 100.
Your Comment