19 Machi 2011 - 20:30

Uhakika huu usiopingika kwamba Iran imeendelea kiteknolojia kiasi kwamba imeweza kuitoa ndege ya kisasa ya kijasusi ya Marekani aina ya RQ-170 katika udhibiti wa Marekani na kuilazimisha kutua nchini Iran baada ya ndege hiyo kuingia ndani ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, umetoa pigo kubwa sana la kiteknolojia kwa viongozi wa Marekani. Hivi sasa viongozi wa Marekani wanatoa maneno yanayogongana kiasi kwamba hawajulikani wanasema nini.

Awali walikanusha kabisa habari hiyo, baadaye wakaanza kukiri hatua kwa hatua, na hivi sasa licha ya kupita siku kadhaa tangu Iran iudhihirishie ulimwengu uwezo wake mkubwa wa kiteknolojia kupitia kuilazimisha ndege hiyo ya kisasa ya Marekani kutua na kuidhibiti nchini Iran, bado viongozi wa Marekani wanaendelea kutoa maneno yanayogongana kuhusu suala hilo. Ingawa juzi Jumamosi, viongozi wa Marekani walidai kuwa ndege hiyo ya Marekani ilianguka nchini Iran kutokana na hitilafu za kiufundi, lakini mtandao wa habari wa utawala wa Kizayuni wa Israel DEBKA umekanusha madai hayo ya viongozi wa Marekani. Mtandao huo ambao una mfungamano wa karibu na mashirika ya kijasusi na kiusalama ya Israel umethibitisha kuwa, Iran imeweza kuitoa ndege hiyo ya kijasusi ya Marekani katika udhibiti wa Wamarekani na kuilazimisha kutua salama usalimini katika ardhi ya Iran. Mtandao huo umesema kuwa, kama madai ya viongozi wa Marekani yangelikuwa kweli, basi ndege hiyo ingekuwa imeharibika vibaya lakini hivyo sivyo ilivyotokea. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa hivi sasa Marekani haina njia nyingine isipokuwa kukiri tu kuwa, Iran ina uwezo mkubwa katika vita vya kielektroniki. Viongozi wa Marekani wanapaswa wakubali pia kuwa, vikwazo vikubwa ilivyowekewa Iran kwa miaka 32 sasa, si tu havijalidumaza taifa hili, lakini pia vimekuwa ni chachu kubwa ya kuweza Iran kupiga hatua kubwa za kimaendeleo. Wataalamu wa masuala ya kijeshi wanasema hakuna majibu mengine isipokuwa kukiri kwamba Iran imeendelea sana katika masuala ya kiteknolojia na katika vita vya elektroniki kwani si jambo jepesi kwa nchi yoyote ile duniani, kuweza kupenya kwenye mfumo wa kudhibiti ndege kama ya RQ-170 ya Marekani ambayo mbali na kuwa haionekani kwenye rada, lakini pia inatumia teknolojia ya kisasa kabisa ya kijasusi na tena hata haimilikiwi na Wizara ya Ulinzi ya Marekani bali ni mali ya shirika la kijasusi la nchi hiyo pekee CIA. Duru za kijeshi zilizonukuliwa na mtandao huo wa DEBKA zimeuliza maswali kadhaa bila ya kupata majibu zikisema kuwa, ndege hiyo ilikuwa na mfumo wa kujiripua yenyewe wakati inapotoka mikononi mwa Wamarekani, lakini hilo nalo halikufanyika na hili halithibitishi kitu kingine isipokuwa uwezo mkubwa wa Iran katika vita vya kielektroniki. Kwa upande wake, gazeti la kila siku la Wall Street Journal la Marekani nalo limeripoti kuwa, awali viongozi wa Marekani walikusudia kufanya operesheni ya kijeshi ndani ya ardhi ya Iran ili kuiharibu-haribu ndege yao hiyo ya kijasusi iliyoingia mikoni mwa Wairani, lakini kwa kukhofia majibu makali ya Wairani waliogopa kufanya operesheni hiyo. Kiujumla ni kuwa, kitendo cha Iran cha kuweza kukata mawasiliano ya ndege hiyo na makao makuu ya kuiongoza na baadaye kuidhibiti ndege na kuiongoza hadi mahala wanapotaka wataalamu wa Kiirani, huku Wamarekani na majigambo yao yote wakishindwa kufanya chochote katika suala hilo, kinatoa ujumbe muhimu sana kwa maadui na marafiki wa taifa la Iran, kwamba taifa hili si la kuchezewa.