19 Machi 2011 - 20:30

China imepinga vikali hatua ya Marekani ya kuiwekea Iran vikwazo vya upande mmoja kutokana na mradi wake wa nyuklia wenye malengo ya amani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hong Lei amesema kuwa Beijing inaamini kuwa mazungumzo ya kidiplomasia ndiyo njia sahihi ya kutatua kadhia ya nyuklia ya Iran. China imeikosoa Marekani kwa kuziweka sheria za ndani ya Marekani juu ya sheria za kimataifa katika kuiwekea Iran vikwazo. Aidha msemaji huyo ametetea biashara ya mafuta kati ya China na Iran na kukosoa vikali nchi za Magharibi kwa kujaribu kuvuruga uhusiano huo wa kibiashara. Hivi karibuni Rais Barack Obama wa Marekani, alitia saini sheria mpya ya kushadidisha vikwazo dhidi ya Iran ambapo hivi sasa imelengwa Benki Kuu na sekta ya fedha ya Iran. Weledi wa masuala ya kimataifa wanaamini kuwa, kuiwekea vikwazo Tehran si suala jepesi la kuweza kufanikiwa kwa kupitisha azimio au kupasisha sheria tu kwani Iran ni kiungo muhimu sana katika suala la nishati ya mafuta ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa dunia na kwamba nchi za dunia haziwezi kutia mkono kizani kufuata kibubusa siasa za kiadui za Marekani dhidi ya Iran.