Umoja wa Ulaya umekubaliana kuweka vikwazo vipya dhidi ya jimbo lililochukuliwa na Urusi la Crimea kuonesha msimamo wake dhidi ya Urusi, wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya wakijitayarisha kujadili mzozo unaoongezeka wa kifedha nchini Urusi huku kukiwa na hofu za athari katika uchumi wa mataifa hayo.
Viongozi hao ambao wanakutana mjini Brussels pia wanaunga mkono mpango wa uwekezaji wa euro bilioni 315 wenye lengo la kuchochea uchumi wa mataifa ya Ulaya unaodorora, licha ya kuwa ahadi za fedha taslimu hazitarajiwi kutolewa.
Mkutano huo wa kwanza kuongozwa na rais mpya wa baraza la Ulaya Donald Tusk , kiongozi wa zamani wa Poland , unakuja huku kukiwa ya hali ya kuporomoka kwa sarafu ya Urusi ya rouble kutokana na vikwazo vya mataifa ya magharibi na kupungua kwa bei ya mafuta.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kabla ya kwenda mjini Brussels kwamba vikwazo vya mataifa ya magharibi dhidi ya Urusi havikwepeki hadi pale rais Vladimir Putin atakaporuhusu Ukraine huru na iliyoungana.
Rais wa Urusi amelihutubia taifa lake na kuwaambia kuwa wasiwe na wasi kwani haya ni matatizo ya muda mfupi tu na kwamba uchumi wa Urusi utakuwa wa hali ya juu muda si mrefu,pia ameituhumu Marekani na Saudia Arabia kwa kushusha bei ya mafuta makusudi kwa lengo la kudhoofisha uchumi wa Iran na Urusi.