28 Januari 2015 - 12:59
Obama, Mfalme Salman waijadili Iran na Daesh

Ujumbe mzito wa Rais Barack Obama wa Marekani kwenda kutoa pole kwa ufalme wa Saudi Arabia baada ya kifo cha Mfalme Abdullah unatajwa kuwa kipimo kwa diplomasia iliyoathirika ya mataifa hayo mawili.

Ujumbe mzito wa Rais Barack Obama wa Marekani kwenda kutoa pole kwa ufalme wa Saudi Arabia baada ya kifo cha Mfalme Abdullah unatajwa kuwa kipimo kwa diplomasia iliyoathirika ya mataifa hayo mawili.

Mara tu baada ya kukutana na mgeni wake, Mfalme mpya Salman al-Saud alituma ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter, akisema kwamba lilikuwa ni jambo la fahari kukutana na Rais Obama, akiongeza kwamba wawili hao walijadili "mafungamano ya kihistoria na ushirika wa kimkakati" kati ya nchi zao katika kuunga mkono amani ulimwenguni.

Lakini kile ambacho Mfalme Salman hakukitaja kuwa kiligusiwa kwenye mazungumzo yao ni rikodi ya haki za binaadamu ya Saudi Arabia, ambayo daima Marekani imekuwa ikisema ina mashaka nayo, ingawa haijawahi kufika umbali wa kutoa matamko ya kulaani vitendo vya ukandamizaji wa serikali dhidi ya raia.

Maafisa wa Marekani walisema Obama alilizusha suala hilo kwa njia ya jumla jamala bila kugusia mkasa wa mwandishi wa blogu, Raef Badawi, ambaye amehukumiwa kuchapwa viboko 1,000 kwa kile ambacho mamlaka za Saudia zinasema ni kuukashifu Uislamu. Adhabu hiyo, ambayo sasa imesitishwa kwa sababu za kiafya, imezusha wasiwasi mkubwa kwenye jamii ya kimataifa.

  Kwa mujibu wa mashirika ya habari ya kimataifa, Rais Obama na Mfalme Salman waliutumia mkutano wao kujadiliana pia suala la programu ya nyuklia ya Iran, nchi ambayo Saudi Arabia inaichukulia jamhuri ya kiislamu ya Iran kama adui yake mkubwa kwenye Ghuba ya Ajemi.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya mazungumzo ilijikita kwenye operesheni ya kijeshi inayoongozwa na Marekani dhidi ya kundi la kigaidi linalojiita Daesh linalofanya jinai zake nchini Syria na Iraq, ambapo Marekani, na Saudia Arabia walikuwa ni wadhamini wakubwa wa kundi hili, kabla halijawageuka na kuwa kinyume nao, ndipo nchi hizi zilipokusanya nguvu ya nchi zingine kukabiliana na kundi hili ambalo hapo awali liliwekwa kwa ajili ya kusabaratisha serikali za Syria na Iraq ambapo hatua hii itakuwa ni kuikata  mabawa Iran na kuidhoofisha.

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani aliyemo kwenye msafara huo alisema viongozi hao wawili walikubaliana kuendelea kuwasaidia wapinzani na magaidi wanao taka kuiangusha serikali ya Syria na pia haja ya kuimarisha umoja wa kitaifa nchini Iraq.

Saudi Arabia ina wasiwasi kwamba kusambaa kwa nguvu na ushawishi wa kundi hilo la Dola la Kiislamu kunaweza kuiathiri moja kwa moja.

Kundi hilo lilitoa mkanda wa vidio mara tu baada ya kifo cha Mfalme Abdullah wiki iliyopita, likishangiria kifo cha yule waliyemuita "Abdullah katili" na kuapa kwamba wataivamia Saudi Arabia hivi karibuni.

Shaka za Saudi Arabia kwa Marekani

Lakini wachambuzi wanasema Saudi Arabia imekuwa hairidhishwi na namna ambavyo Marekani inajitenga na mizozo iliyopo kwenye nchi nyengine za Kiarabu kama vile Yemen na Libya na badala yake imekuwa ikielemea sana upande wa Asia.

Obama ameongoza ujumbe wa watu 29 kutoka vyama vyote viwili vikuu vya kisiasa nchini Marekani, wakiwemo maafisa wa utawala wa zamani wa George Bush, wote wakisema walitaka kuonesha kuunga kwao mkono uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia.

Taifa hilo la Kiarabu ni mzalishaji mkubwa wa mafuta, ambayo sehemu yake kubwa huchimbwa na kuuzwa na kampuni za Marekani.