Shambulio la kombora dhidi ya hospitali mashariki mwa Ukraine limesababisha watu wanne kuuwawa leo, wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani akitarajiwa kufanya ziara mjini Kiev ziara ambayo huenda suala la kuipatia silaha nchi hiyo likawa juu katika ajenda za mazungumzo.
Vifo hivyo vimetokea wakati mbinyo wa jumuiya ya kimataifa kusitisha mapigano unaongezeka ambapo kumeshuhudiwa mamia ya raia wakiuwawa katika wiki za hivi karibuni wakati waasi wanaoiunga mkono Urusi wakisonga mbele katika maeneo yanayoshikiliwa na serikali.
Uwanja wa kuchezea watoto pia ulishambuliwa, mkaazi wa eneo hilo ameliambia shirika la habari la AFP, na maafisa wa serikali wamesema raia wengine wanane wameuwawa katika mapigano katika jimbo hilo katika muda wa saa 24 zilizopita.
Wakati idadi ya vifo inazidi kupanda mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametoa wito wa kusitisha mapigano mara moja kuruhusu raia kuondoka katika eneo la mapigano.
Katika wakati huo huo Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema nchi hiyo haina mpango wa kupeleka silaha Ukraine kupambana na wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Le Drian amesema hayo akizungumzia kuhusu mjadala uliozushwa na ripoti kuwa Marekani inatafakari kuipatia Ukraine silaha. Le Drian amesema msimamo wa Urusi wa kuwapatia msaada wapiganaji wanaotaka kujitenga nchini Ukraine haukubaliki, na amesema mataifa ya Ulaya yanaendelea na vikwazo kutokana na hatua hiyo.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya waasi na Ukraine yamevunjika katika mwezi uliopita, na mapambano mapya ya wapiganaji yanaendelea dhidi ya maeneo muhimu ya mawasiliano na usafiri mashariki mwa Ukraine.