21 Februari 2015 - 10:47
 Mapigano yaendelea mashariki mwa Ukraine

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema vikwazo vipya dhidi ya Urusi ni zingatio ikiwa makubaliano ya amani kumaliza mzozo wa mashariki mwa Ukraine yatakiukwa, ingawa aliongeza kuwa hilo sio lengo.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema vikwazo vipya dhidi ya Urusi ni zingatio ikiwa  makubaliano ya amani kumaliza mzozo wa mashariki mwa Ukraine yatakiukwa, ingawa aliongeza kuwa hilo sio lengo.

Merkel alikuwa akizungumza na waandishi habari pamoja na Rais Francois Hollande leo mjini Paris. Alisema Umoja wa Ulaya unaweza kulizusha suala la vikwazo ikihitajika. Kansela alisema utekelezaji makubaliano ya amani ni mgumu lakini pande zinazohusika zinapaswa kuwajibika.

Wakati huo huo Mapigano yalizuka  tena ijumaa ya jana mashariki mwa Ukraine licha ya juhudi za Ulaya kuhakikisha usimamishaji mapigano unatekelezwa. Jeshi la Ukraine limesema waasi wa wanaopigania kujitenga walivishambulia mara 49 vituo vinavyodhibitiwa na serikali katika muda wa saa 24 zilizopita, wakitumia maroketi , mizinga na magari ya kijeshi. Msemaji wa Jeshi la Ukraine alisema mashambulizi hayo yanaonesha kwamba waasi hawako tayari kuweka chini silaha zao.

 Wakati huo huo waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras ameliambia shirika la habari la Reuters leo, kwamba ana imani ombi la serikali yake kutaka irefushiwe mkopo kwa miezi sita litakubaliwa, licha ya upinzani wa Ujerumani. Tsipras ametoa wito wa kile alichokiita "uamuzi wa kihistoria kufikia makubaliano, kwa mustakbali wa Ulaya." Ujerumani imesema ombi la Ugiriki halitoshi. Ugiriki inakabiliwa na mazungumzo magumu mjini Brussels, na mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro, ili kuweza kupata mkopo na kuepuka kufilisika baada ya muda wa  mpango wa uokozi ambao serikali mpya ya Ugiriki inaupinga, kumalizika tarehe 28 mwezi huu.