24 Februari 2015 - 12:49
Wabunge wa Democratic wamualika Netanyahu

Wajumbe wawili wa ngazi za juu wa baraza la Seneti la Marekani kutokea chama cha Democratic cha Rais Barack Obama, wamemualika Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Wajumbe wawili wa ngazi za juu wa baraza la Seneti la Marekani kutokea chama cha Democratic cha Rais Barack Obama, wamemualika Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwenye mazungumzo ya faragha kukutana na wenzao wakati waziri huyo mkuu atakapoitembelea Marekani hivi karibuni.

Seneta Richard Durbin na mwenzake, Dianne Feinstein, wameonya kwamba kuugeuza uhusiano wa Marekani na Israel kuwa suala la kichama, kunaweza kuwa na athari za muda mrefu.

Maseneta hao wawili wanasema mualiko wao kwa Netanyahu unakusudiwa kudumisha majadiliano kati ya Israel na pande zote mbili za kisiasa kwenye bunge la Marekani, Congress.

Netanyahu anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na uamuzi wake wa kukubali mualiko wa Spika wa Bunge, John Boehmer anayetokea chama cha Republican, kulihutubia bunge hilo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, tarehe 3 mwezi ujao, ikiwa ni wiki mbili tu kabla ya uchaguzi mkuu nchini mwake, na katika wakati ambao ni muhimu sana kwenye mazungumzo kati ya Iran na mataifa makubwa duniani juu ya programu hiyo ya nyuklia.

Wakati hayo yanajiri Jopo la majaji kwenye mahakama moja ya Marekani limekiamuru chama cha ukombozi wa Palestina, PLO, na serikali ya Mamlaka ya ndani ya Palestina, kulipa mamilioni ya fedha kwa wahanga wa Kimarekani. Familia kumi za Kimarekani zinazohusika kwenye kesi hiyo, sasa zitalipwa kiasi cha euro milioni 190 za fidia. Mahakama hiyo imeitia hatiani PLO na serikali ya Palestina kwa kuwapa msaada wa vifaa magaidi. Magaidi hao walitumia vifaa hivyo kwenye matukio sita tafauti ya mabomu nchini Israel, kati ya mwaka 2002 na 2004, ambapo watu 33 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.