Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Mohammed Javad Zarif, ameyashutumu mataifa ya magharibi wa kuchochea itikadi kali za Kiislamu kwa kushindwa kulinda haki za Waislamu wahamiaji.
Mohammad Javad Zarif ameliambia baraza la haki za binadamu la Umoja wa mataifa lenye makao yake makuu mjini Geneva leo kuwa idadi kubwa ya wale wanaojiunga na kundi la kigaidi la Daesh linalojiita Dola la Kiislamu na mengine ni raia wa mataifa ya kidemokrasia ya magharibi.
Amedokeza kwamba baadhi ya wale , ambao wanawachinja raia wasio na hatia wanazungumza lugha za mataifa ya Ulaya kwa ufasaha na lafudhi ya jamii ya mataifa hayo, akimlenga "Jihadi John" ambaye ameonekana katika video kadhaa za kundi la kigaidi la Daesh za propaganda zinazoonesha kuuwawa kwa wafungwa wa kundi hilo.
Jihadi John ametambulika wiki iliyopita kuwa ni Muhammed Emwazi, kijana aliyekulia mjini London. Zarif pia amerudia dai la nchi yake la hapo kabla kwamba juhudi za mataifa ya Ulaya kuhimiza haki za binadamu katika mashariki ya kati zimevuruga tawala zilizopo na kuyanufaisha makundi ya itikadi kali.