15 Machi 2015 - 19:34
 Netanyahu atafuta uungwaji mkono kabla ya uchaguzi

Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya uchaguzi na kupungua uungwaji mkono katika uchunguzi wa maoni

Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya uchaguzi na kupungua uungwaji mkono katika uchunguzi wa maoni, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu leo ametoa wito wa kutafuta uungwaji mkono kwa kujaribu kukivutia chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia Kalanu. Wakati kampeni zikikikaribia kumalizika, Netanyahu alitarajiwa kuzungumza mjini Tel Aviv kwa lengo la kukiimarisha chama chake kinachopungua umaarufu cha siasa za mrengo wa kulia, Likud. Akizungumza na vituo viwili vikuu vya redio nchini Israel, Netanyahu alisema yuko tayari kuukabidhi wadhifa mkuu wa wizara ya fedha kwa Kiongozi wa Kalanu Moshe Kahlon. Kahlon, waziri wa zamani maarufu katika chama cha Likud, na ambaye chama chake kinatabiriwa kushinda kati ya viti vinane na kumi, anatarajiwa kuwa turufu ya kushirikiana na chama kitakachoshinda na kuunda serikaki baada ya uchaguzi huo wa Jumanne wiki ijayo.