Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amerudia onyo lake kali kuhusu uwezekano wa makubaliano ya kinyuklia na Iran leo, akisema dunia inalazimika kusisitiza kupata kile alichosema "makubaliano bora", ambayo yanahusisha kuridhia baadhi ya mambo ili kubadilisha tabia ya uongozi wa Iran.
Wakati wajumbe wa majadiliano wakiendelea na mazungumzo nchini Uswisi siku moja baada ya kuachana na muda wa mwisho wa Machi 31 ili kufikia muongozo wa makubaliano ya kinyuklia, Netanyahu amesema mataifa makubwa duniani yanatafuta njia za kupunguza vikwazo dhidi ya Iran wakati ikiendelea kuleta mtafaruku katika mashariki ya kati na inaitishia Israel kwamba itaiangamiza.
Serikali ya Israel inapinga kabisa makubaliano hayo kwa madai kwamba yataipa Iran nguvu zaidi, ambapo Iran ndio nchi pekee inayopinga bayana uvamizi wa Israel na dhuluma zake kwa wapalestina na kuahidi kuwasaidia wapalestina kuchukua haki zao kwa nguvu za mtutu kama zilivyochukuliwa.
Mazungumzo hayo yameendelea leo wakati Iran ikisisitiza kwamba haitakubali kuharakishwa kuingia makubaliano yasiyofaa ambayo yatashindwa kutimiza haki zake za msingi za kuondolewa vikwazo vyote na kutambuliwa mradi wake wa amani ya nyuklia na kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake.
Wakati huo huo kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ana matumaini maridhiano yatapatikana leo katika mazungumzo ya mataifa makubwa na jamhuri ya kiislamu ya Iran.